Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere (Tazara) umekamilika kwa asilimia 98.
Amesema wakati wowote kuanzia Oktoba, 2018, Rais John Magufuli atazindua barabara hiyo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Jumatano Agosti 29, 2018 mara baada ya kutembelea eneo hilo pamoja na Ubungo ambako itajengwa barabara ya juu (Interchange).
"Nimepata maelezo ya ujenzi wa barabara hii na nimeelezwa umefikia asilimia 98," amesema Majaliwa huku akiwataka kukamilisha haraka asilimia mbili iliyobaki.
Majaliwa pia alibainisha kuwa ukaguzi alioufanya leo ni wa mwisho, “kilichobaki ni kufanya maandalizi ya uzinduzi utakaofanywa na Rais Magufuli."
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutarahisisha usafiri kwa wananchi wanaotoka katikati ya jiji kwenda maeneo ya uwanja wa ndege pamoja na wale wanaotoka Buguruni na Temeke.
Kuhusu ujenzi Ubungo amesema, “tunataka na pale Ubungo kujenga Interchange ili kurahisisha usafiri."
Amesema mpango wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka kutoka mjini kwenda Pugu-Gongo la Mboto na katikati ya jiji kwenda Kongowe-Mbagala ukikamilika utarahisisha zaidi usafiri katika jiji hilo.
Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuratibu mpango huo ikiwamo ujenzi wa barabara za juu eneo la Mwenge na makutano ya Uwanja wa Taifa kwenda bandarini na Morocco, Kinondoni.
Katika ziara hiyo Majaliwa ameambatana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) na viongozi mbalimbali wa Serikali.