Aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma kusini David Kafulila amekanusha uvumi wa madai ya baadhi ya wanasiasa wanaodai uteuzi aliofanya Rais John Magufuli kwa Wakuu wa wizara, Mikoa na Wilaya hivi karibuni ni wa kisiasa na sehemu ya malipo kwa kuwa amewapa nafasi waliotoka upinzani.
Kafulila amekanusha uvumi huo wakati akizungumza katika mahojiano maalum na www.eatv.tv, ambapo amesema taarifa za wanasiasa wanaosema serikali ya CCM imekuwa ikinunua wanasiasa kutoka upinzani kwa ahadi ya kuwapa madaraka ikiwemo katibu tawala, ukuu wa mkoa na wilaya, hazina ukweli wowote na kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kumnunua na kama nikununuliwa ingekuwa wakati wa sakata akaunti ya Tegeta Escrow.
Kafulila ameeleza kuwa hawezi kununuliwa kwa gharama yoyote kwani hakuna wakati watu waligawana fedha kama kwenye sakata la Tegeta Escrow, hivyo huo ndio ulikuwa muda wa yeye kununuliwa na sio sasa.
Amesema jambo kubwa lililomuondoa CHADEMA kwenda CCM ni kukubaliana na yale ambayo yanafanywa na Rais Dkt. John Magufuli katika utendaji wa serikali, usimamizi wa rasilimali, vita dhidi ya ufisadi na katika mambo makubwa ya kimkakati ya namna gani ya kuisogeza Tanzania mbele isiwe tu katika sura ya Afrika Mashariki.
Amesema " hayo ndio mambo makubwa ambayo nilikuwa nikiyapigia kilele ndani ya bunge na katika siasa ndiyo hata ambayo Mh.. rais anafanyanyia kazi kwa hiyo nisingeweza kuendelea kuwa mnafiki wa kupinga wakati yanayofanyika ni yale ambayo nilisema yafanyiwe kazi hilo ni jambo muhimu sana".
Akizungumzia hatma yake kwenye siasa baada ya kuteuliwa kuwa katibu tawala wa mkoa wa Songwe Kafulila amefafanua kuwa kila jambo lina nafasi yake na kamwe hawezi kuchanganya suala la utendaji na siasa.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa sheria ya utumishi atatelekeza majukumu yake ndani ya sheria, hivyo jambo pekee ambalo watanzania wanatakiwa kutarajia ni utekelezaji wa kiwango cha juu kabisa wa maendeleo kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa uma ambayo pamoja na mambo mengine inamtaka mtumishi wa uma kufanya kazi kwa kutoa huduma bora, kutii serikali, bidii ya kazi, kufanya kazi bila upendeleo na kuheshimu sheria.
Ameongeza kuwa "Safari yangu katika siasa ni jambo ambalo siwezi kulijadili sasa kwa sasa mimi ni mtendaji, jambo pekee naweza nikalisema kwa hakika kabisa ni suala la utendaji, tunahitaji pia watu ambao wanajua namna gani ambavyo serikali inafanya kazi sio tu kwamba unakuwa mwanasiasa miaka yote tunahitaji pia kujua namna ya kufanya utendaji"
Kafulila amesema kuwa kwa miaka yote akiwa kwenye siasa amekuwa akikosoa, sasa ni wakati wake wa kutenda yale ambayo amekuwa akikosoa.
Aidha licha ya David Kafulila kushindwa kutetea kiti chake cha Ubunge katika jimbo la Kigoma kusini kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 kwa tiketi ya chama cha NCCR Mageuzi lakini jina lake limebaki kwenye historia ya Tanzania kuwa miongoni mwa wabunge walioisaidia serikali kuibua ufisadi wa kutisha wa shilingi bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow.