Wanasheria wawili wa msanii wa muziki ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, wamesema mwanasiasa huyo ana hali mbaya kiafya kwani hawezi kutembea wala kuzungumza.
Wakiwa pamoja na familia ya Bobi, awali wanasheria hao walizuiwa kumwona mbunge huyo aliyekamatwa Jumatatu mjini Arua pamoja na wanasiasa kadhaa wa upinzani. Alifikishwa katika Mahakama ya Kijeshi mjini Gulu ambako alishtakiwa Alhamisi kwa kosa la kumiliki isivyohalali bunduki na risasi.Lakini pia ushiriki wake kwenye machafuko katika eneo la Arua, yaliyochangia kushambuliwa kwa msafara wa magari ya rais Yoweri Museveni.
Hata hivyo, alishtakiwa mbele ya wanasheria wake wawili; Asuman Basalirwa (Mbunge wa Manispaa ya Bugiri) na Medard Seggona (Mbunge wa Busiro Mashariki).
Kwa mujibu wa Basalirwa, ambaye alikuwemo kwenye chumba cha mahakama, uso wa mteja wake ulikuwa umevimba na hakuwa anaweza kutembea wala kuongea. Seggona alisema Bobi Wine hakuweza hata kuandikisha maelezo kwa sababu alikuwa katika hali mbaya na alikuwa amefungwa pingu.
“Hali ya Kyagulanyi ni mbaya sana. Ana maumivu makali. Hawezi kuzungumza, na anapata shida sana hata kukaa. Uso wake umevimba na hawezi kuona kwa sababu ya mateso aliyopata kutoka kwa askari wa SFC. Hakuweza hata kuzungumza wakati akisomewa mashtaka na naamini hakuwa anajua kinachoendelea wala kuelewa mashtaka aliyosomewa,” alisema Seggona alipozungumza na wanahabari.
Familia yake haikuruhusiwa kuingia kwenye chumba cha mahakama kusikiliza kesi hiyo chini ya mwenyekiti Luteni Jenerali Andrew Gutti.
Barbara Itungo maarufu kama Barbie, ambaye ni mke wa Bobi Wine alianguka na kuangua kilio wakati wanasheria wa mumewe wakielezea namna alivyoteswa.
“Nikiwa mke na mama, uvumilivu wangu uko majaribuni. Serikali iniruhusu nimwone mume wangu. Nina wasiwasi na hali yake kwa sababu najua alipigwa sana na wanajeshi,” alisema huku akitokwa machozi
Hali ya Bobi Wine ni Mbaya, Hawezi Kuongea Wala Kusimama.,...Bado Anashikiliwa na Polisi
0
August 18, 2018
Tags