Hali ya Niyonzima Simba Yafika Pabaya

Hali ya Niyonzima Simba Yafika Pabaya
Upo uwezekano mkubwa wa kiungo mchezeshaji wa Simba Mnyarwanda, Haruna Niyonzima kutimka ndani ya kikosi hicho kutokana na maelewano mabaya na viongozi wake.

Niyonzima aliyejiunga na Simba msimu uliopita akitokea Yanga, amerejea nchini hivi karibuni akitokea kwao Rwanda, hakuwa kwenye kikosi cha timu hiyo kilichoweka kambi ya wiki mbili nchini Uturuki.

Kwa mujibu wa gazeti la Championi, kiungo huyo alitarajiwa kukutana na viongozi wa timu hiyo juzi Alhamisi jioni kwa ajili ya kujadiliana hatma yake Simba. Mtoa taarifa huyo alisema, kiungo huyo ameonekana hana mpango wa kuendelea kuichezea, ni baada ya kutofautiana kwenye baadhi ya makubaliano yaliyokuwepo kwenye mkataba.

“Uwezekano wa Niyonzima kubaki kuendelea Simba kwenye msimu ujao ni mdogo kwani yeye mwenyewe ameonekana hana nia tena kubaki kuichezea timu hiyo. “Hata kurejea kwake jijini Dar kumetia hofu ni baada ya kurejea pekee huku familia yake akiiacha nyumbani kwao Rwanda, hiyo inatosha kabisa kuthitibitisha hilo Niyonzima hataichezea Simba katika msimu ujao.

“Kuna baadhi ya vitu ametofautiana na viongozi katika masuala ya kimkataba ambayo wanayafanya siri, hivyo upo uwezekano mkubwa wa Niyonzima kuusitisha mkataba wake Simba na kurejea kucheza soka nyumbani kwao,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Niyonzima kuzungumzia hilo alisema: “Sipo kwenye nafasi nzuri kwa kuzungumzia hilo suala katika kipindi hiki, jana (juzi Alhamisi) nilitarajia kukutana na viongozi wa Simba kwa kuzungumza nao lakini hilo halikuwezekana. “Nitalizungumza hilo baada ya kukutana na viongozi wa Simba, kwani kichwa changu hivi sasa hakipo sawa kabisa nafikiria familia yangu ambayo ipo nyumbani Rwanda,” alisema Niyonzima.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad