KWA wanamitindo wakali Bongo, Hamisa Mobeto ni moja kati ya warembo ambao wanafanya vizuri na kusumbua kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kazi zake na skendo za hapa na pale.
Lakini kiki kubwa kabisa iliyompaisha ni kuzaa na mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’. Mrembo huyo alizaa na Diamond wakati mkali huyo alipokuwa kwenye uhusiano mzito na mjasiriamali wa Kiganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye naye amezaa naye watoto wawili.’
Ishu ilikuwa hot sana na kuzua tafrani ya aina yake kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Kwenye mitindo Mobeto ameshawahi kushinda tuzo kadhaa nje ya nchi, ikiwemo Tuzo za Starqt kutoka pande za Johannesburg, Afrika Kusini katika kipengele cha Chaguo la Watu.
Pamoja na kufanya shughuli mbalimbali za mitindo, mrembo huyu anamiliki duka lake la nguo lililopo maeneo ya Kijitonyama jijini Dar. Amani limepata nafasi ya kufanya naye mahojiano kuhusiana na mambo mbalimbali yanayomhusu. Karibu uyasome:
Unafanya vizuri katika kazi zako lakini umekuwa ukipondwa sana kwenye mitandao ya kijamii, unafikiri tatizo ni nini?
Unajua kila king’aacho hakiwezi kosa changamoto hasa ukiwa unang’aa sana kuliko mtu mwingine. Mimi huwa sijali, maana naamini ukiona unaongelewa sana jua kuna mazuri mengi unayoyafanya yanawaogopesha wengine kiasi cha kuwafanya wakuandame.
Kama hauna kizuri basi hakuna mtu atakaye kuongelea. Kwa hiyo hizo changamoto zinanifanya nijue kumbe nafanya vizuri na pia zinanijenga kwa namna moja au nyingine ili kuweza kufanya vitu vingi na vizuri zaidi.
Ushawahi kufikiria labda kuwachukulia hatua za kisheria, maana wanakuharibia biashara na heshima yako mbele ya jamii. Kuna wakati nakaa kimya lakini inapozidi huwa nachukua hatua, kwa mfano hivi karibuni kuna mtu alinitukana kwenye ukurasa wake wa Instagram, amekamatwa, natumaini kwa sababu tuna sheria ya makosa ya mitandao na wengine wapenda matusi nitaendelea kuwachukulia hatua.
Umekuwa na uhusiano na Diamond mpaka mmezaa mtoto nje ya ndoa; je, mzazi mwezio huyo akileta mahari utakubali kuolewa naye.
NDIYO NITAKUBALI.
Mbona umekubali haraka namna hiyo, kwani hakuna mwanaume mwingine aliyewahi kuja kutaka kukuoa? Wapo wengi tu ambao wamekuja kutaka kutoa posa lakini kuoana na mtu mnatakiwa muwe na ‘chemistry’ moja, mimi na Diamond tushakuwa na mtoto, lakini nina mwingine pia kama alivyo yeye.
Unadhani kigezo cha kuwa na mtoto naye kinatosha kuwa sababu ya kukubali kuolewa na Diamond? Kinachochea; lakini mpaka yawepo makubalino mengine kwamba atakuwa tayari kulea watoto wote bila kuwabagua, akikubali kwangu hakuna shida.
Vipi kuhusu makwazo yoyote, hakuna linalokusumbua kiasi cha kuutilia shaka uaminifu wa Diamond. Makosa yapo lakini hayo naweza kuyaangalia mbele lakini siyo kwa sasa, kama ni mtu mwenye nia njema na mimi ataonekana.
Mbali na kulea mtoto kuna uhusiano wowote ambao unaendelea kati yako na yeye?
Hahaha! Siwezi kujibu hilo.
Kwa nini huwezi kujibu unaogopa kitu gani?
Kwa sababu ni mambo binafsi sana hayo, siwezi kuyaweka hadharani.
Kuna maneno watu wanasema kwamba hupendi kukosolewa; mtu akikukosoa basi ‘unamfungia vioo’ kwa ‘kumblock’ au kumuondoa kwenye kundi la marafiki zako mitandaoni?
Sijawahi wafanya hivyo bila sababu, wanashindwa tu kuongea ukweli. Sasa kama mtu kila siku anakuja kwenye ukurasa wangu kunitukana, mtu kama huyo mimi wa nini sasa? Si bora nimblock; ya nini nimwache mtu kama ananipa kero?
Nimalizie kwa swali hili, hivi ile sauti inayosikika kwenye wimbo wa Jibebe (I like it) wa Diamond ni yako?
Hahah! Jamani si mkamuulize mwenyewe Diamond mimi siyo nafasi yangu kulizungumzia hilo.
Asante kwa muda wako Mobeto.
Asante karibu tena.