Hapi Ataja Sababu za Kufeli Kinondoni

Hapi ataja sababu za kufeli Kinondoni
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi, amesema kuwa mfumo wa ukusanyaji mapato ni wa kizamani 'analog' ndio sababu ya halmashauri nyingi kufeli katika awasilishaji sahihi wa takwimu sahihi za mapato, na kuahidi kubadili mfumo wa ukusanyaji mapato mkoani kwake.

Akizungumza na East Africa BreakFast ya East Africa Radio, leo Jumatatu Agosti 6, 2018 Hapi amesema kuwa kwenye suala la mapato kuna matatizo mawili ambayo ni mifumo ya kizamani ya ukusanyaji pamoja na mfumo wa wataalamu kuziweka takwimu ni mbovu kwakile alichodai kuna watumishi huzifungia kwenye makabati takwimu za mapato, na kudai kuwa takwimu zilizowasilishwa kwa Rais hazikuwa sahihi.

“Kauli ya Rais ilikuwa ni maelekezo lakini, ukweli ni kwamba taarifa zilizofika kwa Rais hazikuwa sahihi kwani takwimu sahihi zipo na zitafikishwa upya”, amesema Hapi.

Agosti 1, 2018 baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa wapya, makatibu wakuu wa wizara na manaibu wake, pamoja na makatibu tawala wa mikoa Rais Dkt. Magufuli aliusifu mji wa Dodoma ambao hivi karibuni aliupa hadhi ya kuwa jiji akisema umeongoza kwa ukusanyaji wa mapato, huku akidai kuwa jiji la Dar es salaam kuna wizi wa mapato huku Kinondoni ikishika nafasi ya mwisho, wilaya iliyokuwa ikiongozwa na Ally Hapi.

“Sasa unaweza ukajua kwamba, hapa Dar es Salaam kuna upigaji tena wa nguvu. Lakini viongozi wapo, na hata Wilaya ya Kinondoni aliyekuwa anaiongoza (Ally) Hapi ndiyo imekuwa ya mwisho, sasa nikawa najiuliza sijui nimtumbue hapahapa au? Kweli wala sifichi, nikasema wilaya ilikuwa ya upinzani ile. Lakini hivi vitu vinatia aibu,” alisema Rais.

Agosti 3, 2018 wakati akiwaapisha Wakuu wa Wilaya wapya na kuwaaga walioondoka Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda alimuagiza Katibu tawala wa mkoa kuhakikisha kuwa takwimu zinapitiwa upya na kuhakikisha zile ambazo hazikuwa sawa ziwekwe sawa ili zifike kwa Rais, kwani hakubaliani na suala la kuzidiwa mapato na jiji la Dodoma.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad