Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kwa sasa hakiwezi kuzungumza jambo lolote linalohusiana na sakata la uchaguzi, kwa kile walichodai wanataka kufanya mkutano wa kamati kuu wenye lengo la kutathimini chaguzi hizo na kutoa msimamo wao kuelekea chaguzi zijazo za marudio.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Vicent Mashinji wakati alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv asubuhi ya leo Agosti 14, 2018, ikiwa imepita siku moja tokea kulipomalizika kwa uchaguzi mdogo wa marudio wa jimbo la Buyungu mkoani Kigoma ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Mhandisi Christopha Chiza kutoka CCM kuwa mshindi wa kiti cha Ubunge katika jimbo hilo.
Mhandisi Christopha Chiza alipata jumla ya kura 24,758 huku mpinzani wake ambaye walikuwa wakichuana vikali kutoka CHADEMA, Elias F. Michael kupata kura 16,910.
"Kwa sasa tunategemea kufanya tathimini ya uchaguzi uliokwisha fanyika siku ya Jumapili pamoja na huo ambao unakuja mwezi Septemba, katika Jimbo la Ukonga na Monduli. Kwa hiyo baada ya tathimini hiyo ndio tutaweza kutoa msimamo wa chama kama tutashiriki kwenye uchaguzi ujao au laa", amesema Dkt. Mashinji.
Kauli hiyo ya Dkt. Vicent Mashinji imekuja baada ya kutokea mivutano mingi kwenye mitandao ya kijamii iliyokuwa ikizungumzia uchaguzi huo wa marudio ambapo baadhi ya watu walidai kutoridhishwa na hali ya uchaguzi mzima.
Septemba 16 mwaka huu kutafanyika uchaguzi mwingine mdogo wa marudio katika majimbo matatu ambayo ni, jimbo la Korogwe vijijini kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Stephen Ngonyani, jimbo la Ukonga na Monduli, kutokana na waliokuwa Wabunge wa majimbo hayo, Mwita Waitara na Julius Kalanga kujiuzulu uanachama wa CHADEMA na kwenda CCM mapema ndani ya mwezi huu Agosti.