Hatma ya vyama vya upinzani 2020 yaanikwa
0
August 05, 2018
NA ISMAEL MOHAMED
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania wamedai kwamba, vyama vya upinzani bado vina nafasi kubwa kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020 na wala haviwezi kufa, licha ya kuwa wanachama wake wengi kukimbilia katika chama tawala cha CCM.
Hayo yamebainishwa na mchambuzi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Benson Bana pamoja na Michael Bante wakati walipokuwa wanazungumza na www.eatv.tv katika nyakati tofauti, baada ya kuwepo wimbi kubwa la Wabunge na Madiwani wa vyama vya upinzani kung'atuka kwenye majimbo yao, kwa kile wanachodai kuenda kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kuijenga nchi.
"Upinzani hauwezi kufa hata siku moja, ila unaweza kudhofika na mimi ninaamini kabisa kwa aina hii ya utendaji wa serikali ya awamu ya tano, kura za upinzani zitapungua kabisa. Wabunge na Madiwani watakuwa wachache sana, Magufuli alichofanya ni kuua vyama vya upinzani kisayansi kwa kutekeleza vile vyote ambavyo viliahidiwa na vyama vya upinzani katika kipindi cha uchaguzi", amesema Bante.
Pamoja na hayo, Bante ameendelea kwa kusema "kinachosababisha wabunge na madiwani kuhama upande mmoja na kuelekea sehemu nyingine ni kutokana na kubaini zile ajenda zao walizokuwa wakizifanyia kazi, zinafanywa na mtu mwingine. Sasa mtu kama huyu abaki sehemu hiyo kufanya nini".
Kwa upande wake, Dkt. Bana ametoa mtazamo wake juu ya muenendo wa hali ya kisiasa nchini kwa kusema mtu anapohama kutoka chama kimoja kuelekea kingine basi isichukuliwe kama anatengeneza mazingira ya uadui au kutaka kuudhofisha demokrasia.
"Watu wengi wanaangalia mfumo huu wa vyama vya vingi ni kama sehemu ya kujenga demokrasia, kwa hiyo vyama vya siasa na upinzani visipokuwepo kuwa tutarudi nyuma kisiasa hiyo sio kweli. Mtu kuhama chama kimoja kwenda kingine ni haki yake ya kikatiba", amesema Dkt. Bana.
Kwa kipindi cha takribani miaka mitatu tayari wabunge watano wameshajivua nyadhifa zao, ambapo dimba lilifunguliwa na Lazaro Nyalandu kutoka CCM kwenda CHADEMA, Maulid Mtulia CUF kuelekea CCM, Godwin Mollel CHADEMA kwenda CCM, Waitara kutoka CHADEMA kurudi CCM pamoja na Julius Kalanga kutoka CHADEMA kurudi CCM.
Wasikilize hapa chini wachambuzi hao wakizungumza kwa undani zaidi juu ya sakata hilo.
Tags