Aliyekuwa naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi, (CUF) Julius Mtatiro ametangaza kuachana na chama hicho ambapo amesema kuwa amefanya hivyo ili kufanya siasa za maendeleo ili kumsaidia Rais Magufuli.
Mtatiro ametangaza kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) leo Agosti 11, 2018 wakati akizungumza na vyombo vya habari ambapo amesema kuwa ameanza kwa kuzungumza na waandishi na kutangaza azma yake ambayo ameitafakari kwa muda mrefu kabla ya kuwataarifu viongozi wa CCM ambao amewaomba wampokee.
“Nawaambia Watanzania kwamba kuanzia leo nitaanza kufanya siasa za maendeleo ili kumsaidia Rais John Pombe Magufuli ", amesema Mtatiro.
Mtatiro ameongeza kuwa , "Nimejiridhisha kwa hitaji la nafsi yangu kwamba nijiunge na Chama cha Mapinduzi CCM, nawajulisha watanzania rasmi kuwa nimeanza mipango ya kutekeleza hili mara moja".
Mtatiro amesema kuwa masuala ya misimamo yake ya sera na ilani za CUF na misimamo ya CUF hayo yanabakia CUF, hivi sasa yeye ni Mtatiro ambaye anajiandaa kujiunga na Chama cha mapinduzi CCM kama mwananchi na anatumia haki yake kikatiba.
Wimbi la viongozi na wanachama wa upinzani kutimkia CCM, lilianza kushamiri mwaka jana ambapo mpaka sasa jumla ya wanachama milioni mbili wameshajiunga na chama cha mapinduzi kuanzia Januari mwaka 2017 hadi sasa kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole.