Baada ya kuwepo na wimbi la viongozi waliochaguliwa na wananchi kuongoza hasa nafasi za udiwani na ubunge kutoka upinzani kuhama vyama na kwenda CCM, historia inaonyesha wale waliohama wengi wao siyo chimbuko la upinzani.
Historia ya Wabunge watatu kutoka CHADEMA mpaka sasa ambao wameshajiuzulu onaonyesha kwamba kabla ya kuingia kwenye chama hicho cha upinzani walishawahi kushika nyadhifa tofauti tofauti ndani ya CCM hivyo sasa hivi kujivua nafasi zao ndani ya CHADEMA ni kama kurudi nyumbani.
Mbunge wa kwanza CHADEMA kujiuzulu alikuwa Dk. Godwin Oloyce Mollel, Mbunge wa Siha ambaye alijiuzulu Disemba 14, 2017. Kwenye historia ya siasa Dk. Mollel aliwahi kuwa ndani ya CCM na kushika nafasi kadhaa ndani ya UVCCM wilaha ya Siha na kuwa kijana mwenye ushawishi ingawa ndani ya Chama chake hicho hakupata nafasi ambayo ingemfanya aweze kuwatumikia wananchi wa Siha.
Hata hivyo, mwaka 2015 Dkt Mollel aliondoka rasmi ndani ya CCM na kutangaza kujiunga na CHADEMA ambako alifanikiwa kugombea ubunge wa Siha na kushinda dhidi ya mpinzani wake wa CCM, Agrey Mwanri na mwaka 2017 aliamua kujivua nafasi yake ya uongozi kwa kumuunga mkono Rais MagufulI.
Mbunge wa pili upinzani kujiuzulu alikuwa Mwita Waitara ambaye yeye kihistoria alijiunga CCM mwaka 1998 ambapo alishika nafasi mbalimbali ndani ya Chama hicho kama vile Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa Tanga kwa nafasi hiyohiyo na kupanda ngazi kuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tanga na baadaye aliporudishwa Dar es Salaama kama Mwenyekiti Msaidizi UVCCM Taifa ndipo alipohama chama hicho na kuingia CHADEMA mwaka 2008.
Baada ya 2008 ya kukosa ridhaa ya Chama ya kuweza kugombea jimbo la Tarime la aliyekuwa Mbunge Marehemu Chacha Wangwe, na 2010 kubwagwa kwenye boksi la kura na mgombea wa CCM, Nyambari Nyangwine, Waitara alirudi kujiimarisha Dar es Salaam Ukonga ambapo 2015 wana-Ukonga walimpa ridhaa ya kuwaongoza na ndani ya takribani miaka miwili na nusu ameamua kurejea nyumbani CCM.
Waitara amejiuzulu nafasi zake za uongozi ndani ya CHADEMA na Ukonga Julai 28, 2018 kwa madai ya kuhofia kupotezwa baada ya kuwa na ugomvi na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe huku nafasi ya Uenyekiti wa chama ukitajwa kama chanzo.
Aidha Mbunge mwingine kutoka CHADEMA mwenye asili ya CCM aliyejiuzulu ni Julius Kalanga ambaye yeye kihistoria ni kiongozi aliyekulia kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi na baadaye alihamia CHADEMA kutokana na upepo wa siasa ulivyokuwa.
Kalanga aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya UV-CCM wa Wilaya Monduli ya mwaka 2007-2012 na Diwani wa Kata Sepeku wilayani humo mwaka 2010 kupitia chama hicho hicho.
Hata hivyo Kalanga alitajwa kati ya makada wa CCM waliokuwa wamejiandaa kuchukua jimbo la Monduli 2015 baada ya aliyekuwa Mbunge, Edward Lowassa kutangaza nia ya kustaafu nafasi hiyo na hata Lowassa alipojiunga na CHADEMA baada ya jina lake kukatwa kwenye kura za maoni Kalanga alihama naye jambo ambalo lilimfanya kushinda kwa urahisi jimbo la Monduli kwa tiketi ya CHADEMA ambapo baada ya kuhudumia kwa takribani miaka miwili na nusu, Julai 31, 2018 ameamua kuvunja mkataba na wana-Monduli na kurejea nyumbani CCM.
Kwa historia ya upinzani wa Tanzania bado wapo Viongozi na wanachama wengi wenye asili ya CCM na wameshikilia nyadhifa mbalimbali je tutegemee na wao kurejea katika machibuko yo?