Hizi Hapa Rekodi 4 za DC Jokate

Hizi Hapa  Rekodi 4 za DC Jokate
JULAI 28, mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alimteua aliyekuwa mshindi wa pili wa mashindano ya ulimbwende Tanzania (Miss Tanzania 2006), Jokate Mwegelo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.

Jokate amechukua nafasi ya aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo, Happyness Seneda William ambapo kabla ya kuchukua nafasi hiyo aliwahi kuwa Kaimu Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Tayari Jokate ameanza kutumikia wilaya yake baada ya kuapishwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo. Ukiachilia kuwa Mkuu wa Wilaya (DC), Jokate ambaye ni mjasiriamali, mwigizaji na msanii wa Bongo Fleva ameweka rekodi 4 na Showbiz Xtra linaanika rekodi hizo;

FILAMU

Mwaka mmoja baada ya kuchukua nafasi ya pili ya Miss Tanzania nyuma ya Wema Sepetu aliyeshinda kipindi hicho, Jokate aliamua kujiingiza katika filamu na ya kwanza kuigiza ilikuwa Fake Pastors kwa ushirikiano na waigizaji wenza Vincent Kigosi, Lisa Jensen pamoja na marehemu Adam Kuambiana.

Mbali na kuigiza filamu nyingine nyingi kama vile From China With True Love ya 2008, Jokate anashikilia rekodi ya kuwa mlimbwende wa kwanza Bongo kufanya filamu ya kimataifa kuhusu elimu. Filamu hiyo inaitwa Chumo iliyotoka 2010 iliyoandaliwa na Shirika la Habari la Kimataifa kuhusu elimu ya juu ya Ugonjwa wa Malaria (Media for Development International).

Filamu hiyo pia imempatia Jokate Tuzo ya Zanzibar International Film Festival (ZIFF) kama mwigizaji bora wa kike 2011 ambapo pia shirika hilo, 2014 lilimtuza kuwa muigizaji bora kwa lugha teule ya Kiswahili.

MUZIKI

Alianza kama utani kwenye Muziki wa Bongo Fleva baada ya kutoa Wimbo wa Kaka Dada 2013 akiwa amemshirikisha Prodyuza Lucci.

Licha ya muziki wake kutoufanya ‘siriazi’ kivile, 2015 aliibuka tena na kuweka rekodi ya kuwa mlimbwende wa kwanza kufanya kolabo ya kimataifa baada ya kutoa Wimbo wa Leo Leo akiwa amemshi-rikisha staa wa muziki kutoka Nigeria Ice Prince. Awali hakukuwa na mlimbwende aliyewahi kufanya kolabo ya kimataifa.

UJASIRIAMALI

Inaeleweka kuwa kila mwaka jarida maarufu la Forbes ambalo hufuatilia maisha ya watu maarufu duniani na kutoa takwimu mbalimbali zikiwepo wanaoingiza pesa nyingi zaidi duniani, mastaa wanaoongoza kwa malipo ama wajasiriamali wa kutazamiwa.

Juni, mwaka jana, Jarida la Forbes Africa lilitoa listi ya wajasiriamali 30 wenye ushawishi Afrika wenye umri chini ya miaka 30 ambao wamefanya mabadiliko makubwa kwenye sekta zao na wanaendelea kufanya vizuri kama wafanyabiashara wenye umri mdogo ambapo Jokate aliweka rekodi ya kuwa miongoni mwa waliotajwa.

Ukiweka pembeni, Jokate anashikilia rekodi ya kuwa mlimbwende wa kwanza Bongo kuingia mkataba mnono wenye thamani ya shilingi bilioni 8.5 za Kitanzania na Kampuni ya China ya Rainball Shell Craft kwa ajili ya kuzalisha na kuuza bidhaa mbalimbali za Lebo ya Kidoti. Jokate amejikita zaidi katika ujasiriamali wa nywele, kandambili pamoja na mabegi ya mgongoni ambayo yote yapo chini ya lebo yake hiyo ya Kidoti.

MICHEZO

Mwaka jana, Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) lilimteua Jokate kuwa balozi mwema wa kujitolea-mpira wa kikapu awapo ndani na nje ya nchi. Katika kutekeleza hilo, alifanikiwa kujenga kiwanja cha mpira wa kikapu Shule ya Jangwani jijini Dar na kumpatia dili la kuungwa na watu wa NBA Afrika.

Kutoka na hilo, ameweka rekodi ya kuwa mlimbwende wa kwanza kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa NBA Afrika, Amadou Gallo aliyewahi kuja nchini kwenye mashindano ya Junior NBA na kumpa shavu la kwenda Marekani kuhudhuria mchezo mkubwa wa kikapu NBA All-Star Game.

Katika usiku huo, Jokate aliweka rekodi nyingine ya kuwa mlimbwende wa kwanza kukutana na kuongea na mastaa wakubwa akiwemo mchezaji mkongwe wa Klabu ya Arsenal, Thierry Henry pamoja na mastaa wa Muziki kutoka Marekani, Beyonce na Jay Z.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad