Hizi Hapa Swaga za Wanamuziki wa Bongo Flava Jukwaani Zinazotia Kichefuchefu


Wanamuziki wa sasa wanabadilika nywele na mavazi tu. Lakini kinachofanyika jukwaani ni kile kile alichokifanya Inspekta Haroun miaka 17 iliyopita. Tena yawezekana LWP walikuwa bora zaidi kwa sababu hawakuiga swaga za Juma Nature, kuliko hawa ambao wanafanya alichofanya Nature miaka hiyo.

Kwenye jukwaa la Fiesta miaka 18 iliyopita Profesa Jay, akiwa tayari ana dakika 30 jukwani akivuta pumzi kabla ya kuendelea na shoo aliuliza mashabiki: “Tuendelee ama tusiendelee?” Swali lilienda sambamba na biti kurusha watu, mashabiki wakiitikia “Tuendelee.” Alikuwa akicheza na jukwaa kunogesha shoo.

Leo hii mwanamuziki kaimba wimbo mmoja wenye ‘vesi’ mbili tena fupi kama video za insta, tayari anaanza kuuliza mashabiki “Tuendelee ama tusiendelee?” Huu ni ‘uwaki’ wa kiwango cha lami. Mwanamuziki hajaanza hata kuimba wimbo tayari anawashurutisha mashabiki eti “Piga keleleeee.” Hizo zilikuwa mbinu za nyakati zile kuamsha mizuka ya mashabiki. Wakati ule mwanamuziki anagonga nyimbo tano zenye ‘vesi’ tatu tena ndefu. Mashabiki wanasikiliza mistari kuliko midundo wala viuno, ndipo swaga za piga kelele au tuendelee ama tusiendelee zikaja.

Mashabiki wa kizazi hiki wagongee ngoma tu watapiga kelele na watataka uendelee ama usiendelee. Mambo ya “Upande huu siwasikii.” Mambo ya kale sana. Yanachosha maana yameshafanyika sana majukwaani toka enzi za kina Remmy Ongala.

Toka enzi za Dj Bonny Luv mpaka katika dunia ya kina Dj Tass, bado mwanamuziki yuko jukwaani anaanza kubishana na Dj, “Yo yo Dj gonga track number tatu.” Manaake mpaka anapanda jukwaani hakujiandaa. Kwenye ulimwengu ambao hautegemei CD tena.

Afande Sele alizidiwa pale Uwanja wa Uhuru 2004, akazimia jukwani baada ya kukaidi ushauri wa Daktari aliyemuonya asifanye shoo baada ya kugundua ana wadudu wa malaria kama wote. Leo hii eti Lavalava naye anazimia jukwaani baada ya kupigwa busu na shabiki wa kike. Busu lenyewe la utosini.

Hii inatokana na wanamuziki kukosa muda wa kujifunza kwa wenzetu. Wako bize kuchat na madem mitandaoni badala ya kutazama wenzao duniani wanafanya nini kwa sasa. Matokeo yake wanarudia alichofanya Stara Thomas maika hiyo. Jifunzeni.

I
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad