Jamii imetakiwa irudi katika dini zao pamoja na kurudisha malezi ya zamani kwa lengo la kupunguza au kuondoa kabisa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Hayo yameelezwa na mkuu wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa kusini Ali Mohammed Othmani wakati akitoa elimu juu ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanafunzi wazazi,walezi pamoja na walimu huko makunduchi mkoa wa kusini unguja.
Amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa kusini unaongoza kwa kesi za udhalillishaji ikiwemo kubaka,kulawiti na mengineyo jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi na kushuka kwa kiwango cha elimu pamoja na kushuka nguvu kazi ya taifa.
Nae afisa wa dawati la jinsia na watoto shuwekh Zuberi amefafanua madhara ya ukatili ambayo yanaweza kumpata muathirika wa tatizo hilo ni pamoja na kuathirika kisaikolojia, kupata ulemavu na hata kupata maumivu makali katika mwili wake.
Kwa upande wake diwani wa wadi ya makunduchi Zawadi Hamdu amewashukuru dawati la jinsia kwa kuja kutoa elimu na amewataka wawe mstari wa mbele katika kushulikia kesi zao ili kuweza kupatiwa hukumu mapema.