KWELI; usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Ishu ya Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu kutokuzaa imepindishwapindishwa weee, kumbe ana gonjwa linalomzuia kunasa ujauzito.
Nani kasema? Ni Wema mwenyewe ndiye aliyefunguka hivi karibuni mbele ya ‘mshika kalamu’ wa Risasi alipokuwa akifanya naye Exclusive Interview nyumbani kwake Salasala jijini Dar es Salaam.
“Karibu uketi.” Hivi ndivyo safari ya mahojiano kati ya mwandishi wetu na miss huyo ilivyoanza na kuwafikisha katika kuzungumzia suala la mrembo huyo kutokuzaa mpaka sasa.
HAYA HAPA MAHOJIANO
Risasi: Pole na kuumwa maana leo ndiyo tunaonana.
Wema: Asante sana, niliumwa siyo mchezo.
Risasi: Ndiyo hiyo ishu ya kukatwa utumbo?
Swali hili lilizingatia habari zilizozagaa mitandaoni kwamba mrembo huyo alikwenda nchini India kufanyiwa oparesheni ya kukatwa utumbo ili kupunguza mwili na kujenga muonekano mzuri.
Wema: (Mshangao) kukatwa utumbo tena? Unajua mimi sijakatwa utumbo kama watu wanavyosema; ningekatwa nisingekuwa hivi.
Risasi: Nini sasa kilikuwa kikisumbua maana kuna wakati ulikwenda India kwa matibabu?
Wema: Unajua mimi nilikuwa na tatizo kubwa sana kwa upande wa tumbo langu la uzazi lililosababisha nisiweze kuzaa kwa muda wote huu.
Risasi: Pole sana; tatizo lililokuwa linasababisha usizae! Ni tatizo gani hilo?
Wema: Ngoja niweke wazi leo watu wajue, mimi nina ugonjwa ambao unasababisha mayai yangu ya uzazi kutoboka na kushindwa kupevusha mbegu za uzazi.
KIPINDI CHA KULITAZAMA GONJWA HILO
Mara baada ya Wema kufichua siri tatizo linalomzuia kuzaa na kwamba walioligundua ni madaktari wa nchini India ambako alifanyiwa upasuaji Risasi lilitaka kujua ugonjwa huo unaitwaje.
Kwa sababu Wema mwenyewe alishindwa kufafanua undani wa ugonjwa wake, dalili zake, visababishi, tiba na kinga yake, Risasi liliuweka kuwa ‘asaimenti’ ya kuifanyia kazi kupitia madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake.
TUENDELEE NA MAZUNGUMZO
Wikienda: Kwa hiyo video uliyokuwa ukionekana uko hospitali hapa Bongo ilikuwa ni nini?
Wema: Unajua baada ya oparesheni ya India niliporudi nikapata tatizo la kushindwa kupumua vizuri na kingine nikapata maambukizi ya bakteria kwenye kidonda na presha ikawa inashuka.
Risasi: Oooh! Kwa hiyo baada ya upasuaji huko India tatizo la mji wa uzazi limeisha?
Wema: Naendelea na matibabu lakini tatizo limeanza kupungua nafikiri baada ya mwaka nitakuwa mzima kabisa.
ISHU YA KANSA YAIBUKA
Risasi: Risasi linakuombea heri ugonjwa huo uweze kuisha na kukurejeshea furaha.
Wema: Nashukuru ila kiukweli hali ilikuwa mbaya sana, maana madaktari wa India waliponifanyia vipimo walisema kama ningechelewa kuutibu ugonjwa uliokuwa unanisumbua ungeweza kubadilika na kuwa kansa na hivyo kuhatarisha maisha yangu.
Risasi: Duh, kwa hiyo baada ya oparesheni kufanikiwa wamekuhakikishia kuwa hatari hiyo haipo?
Wema: Yeah; hakuna kitisho hicho tena, hali imerudi kawaida kabisa.
DAKTARI AUTAJA UGONJWA WA WEMA
“Kama Wema ameeleza kuwa amekuwa na tatizo kwenye via vyake vya uzazi na kwamba mayai yamekuwa yakishambuliwa na virusi kiasi cha kushindwa kupevuka basi ni kweli lakini nimsahihishe tu kwamba huwa mayai hayatoboki bali huweka vimbe ndogondogo nyingi kwenye yai,” anasema Dokta Godfrey Chale daktari maarufu wa Muhimbili.
Anaendelea kueleza: “Tatizo hilo kitaalamu huitwa Polycysitic Appearing Cyst na ugonjwa huitwa Polycystic Ovarian Disease (PCOD). “Uvimbe wa aina hii unakuwa umezungukwa na vijivimbe vingine vidogovidogo na siyo matobo na huonekana hata kwa wanawake wenye afya njema au wale wenye matatizo ya homoni.
Tokeo la picha la Polycystic Ovarian Disease (PCOD)
“Dalili kubwa ni mwanamke kukosa hedhi, kukosa hamu ya tendo la ndoa, huwa na homoni nyingi za kiume kuliko za kike na wengine kuota ndevu au vinyweleo vingi mwilini na mara nyingi huwakumba wanawake wanene.
“Lakini mwanamke pia anaweza kuwa na uvimbe unaojulikana kitaalamu kama Follicular Cyst. Hii hutokea wakati ovulation (uchavushaji wa yai) isipotokea au baada ya kiungo kiitwacho corpus luteum (kondo la uzazi) kuanza kusinyaa na kupotea yenyewe baada ya kutokupachikwa kwa yai kwenye kuta za mfuko wa kizazi.
“Uvimbe huu unakuwa na wastani wa inchi 2.3 kwa upana, uvimbe huu husababisha maumivu makali sana katikati ya mzunguko wa hedhi yaani siku ya ovulation.“Maumivu haya yanayojulikana kama mittelschmer huonekana kwa wanawake kwa kiwango cha robo moja wenye aina hii ya uvimbe. Kwa kawaida, uvimbe huu hauna dalili zozote.
“Uvimbe kwenye mayai ya mwanamke (ovary) hutokana na mkusanyiko wa majimaji yanayozungukwa na kuta nyembamba ndani ya mayai ya mwanamke. “Uvimbe huu ambao hupatikana ndani ya mayai ya mwanamke ndiyo unaojulikana kama ovarian cyst.
“Kwa kawaida mwanamke anakuwa na mayai mawili katika mwili wake.Yai moja upande wa kulia na yai jingine upande wa kushoto kwake. “Mayai haya hupatikana pembezoni mwa mfuko wa uzazi (uterus). Mayai haya ya mwanamke huanza kuzalisha mayai ya uzazi yanayojulikana kama ovum,” alisema Dk. Chale.
TIBA YA PCOD NI NINI?
Akizungumzia tiba ya Dk Chale alisema: “Mwanamke mwenye vivimbe kwenye mayai yake hutibiwa kwa dawa kwa muda mrefu na mara nyingi hutumia dawa za kisukari aina ya Matfoam. Endapo matumizi ya dawa yatashindwa kuondoa tatizo basi hatua ya kufanyiwa upasuaji huchukuliwa kwa lengo la kuviondoa vivimbe hivyo kwenye mfuko wa uzazi.
Tokeo la picha la WEMA
WEMA ANAWEZA KUZAA?
Kwa mujibu wa daktari huyo, mgonjwa yeyote anapopewa matibabu sahihi na yeye kuzingatia ushauri wa kitalaam atakaopewa basi uwezekano wa kuweza kuzaa upo kwa kiwango kikubwa, lakini kama tatizo halijatibiwa mwanamke hata atembee na wanaume mia ni nadra sana kupata ujauzito. “Kama Wema amefanyiwa upasuaji na anazingatia ushauri wa madaktari wake atapona kabisa na ataweza kupata ujauzito bila wasiwasi,” alisema Dokta Chale.
Tatizo la Wema kutokuzaa limekuwa likipata nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari huku kukiwepo na taarifa kinzani kuhusu mrembo huyo aliyepita kwa wanaume wengi kutofanikiwa kuzaa. Miaka miwili iliyopita katika mahojiano yake na redio moja jijini Dar, Wema aliwahi kukaririwa akisem: “Maneno ya mimi kutokuzaa yananiumiza sana, lakini Mungu hajapenda na sina la kufanya.”
Baada ya miss huyo kusikika akisema maneno hayo, msanii mwenzake wa filamu Riyama Ally alimfariji kwa maneno haya: “Naomba hapa unisikie kwa makini; Nabii Ibrahim alimzaa Nabii Ismail (Isaka) akiwa mzee.”