Idadi ya madiwani na wabunge wa vyama vya upinzani, wengi wao wakiwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wanachi (CUF) waliojiuzulu na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) imefikia 138 nchini Tanzania.
Takwimu zilizotolewa na gazeti la Mtanzania zinaonyesha tangu mwaka 2016 hadi 2018 idadi ya madiwani wa Chadema waliojiunga CCM imefikia 129 huku CUF ikifikia tisa.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania Jumapili, Kitengo cha Habari cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kimeeleza kuwa katika uchaguzi mdogo ujao utakaofanyika Septemba 16, unaojumlisha kata 23 Tanzania Bara, Chadema kina kata 15 za madiwani waliojiuzulu, akiwamo Diwani wa Monduli Mjini ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Isack Joseph maarufu kwa jina la Kadogoo.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikuwa na idadi ya madiwani waliojiuzulu na kusababisha uchaguzi mdogo uliofanyika Agosti 12, mwaka huu ukijumlisha kata 36 kutoka kata 77 zilizotangazwa awali baada ya madiwani 41 kupita bila kupingwa.
Akizungumza na Mtanzania Jumapili, Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt Vicent Mashinji, alisema katika uchaguzi huo, idadi ya madiwani wao waliojiuzulu na kujiunga CCM walikuwa 54.
Kwa upande wa CUF, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi (kambi ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad), Mbarala Maharagande, aliliambia Mtanzania hadi sasa idadi ya madiwani wao waliohama imefikia tisa.
Jumamosi gazeti moja la kila siku liliandika kuwa juzi pekee kulikuwa na madiwani saba kutoka kata za mkoani Pwani waliohamia CCM wakitokea vyama vya upinzani.
Gazeti hilo liliwataja majina na kata zao katika mabano kuwa ni Ally Mbwana (Ikwiriri), Abdul Omari (Kisiju), Sultan Waziri (Njia nne), Issa Salum (Magindu), Shabashaba (Ruvu), Hassan Mohamed na Hamis Mbonde.
Pia idadi aliyoitaja Maharagande inamjumuisha aliyekuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mussa Kafana, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiwalani, aliyejiuzulu juzi na kuomba kupokewa CCM.
Kafana alipishana siku kadhaa na aliyekuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala ambaye pia alikuwa Diwani wa Kata ya Vingunguti (CUF), Omary Kumbilamoto, aliyehamia CCM mwezi Julai, limeripoti Mtanzania.
Limesema kuwa sababu za madiwani hao kujiondoa Chadema hazitofautiani kwa sababu wamekuwa wakitoa hoja kuwa wanahamia CCM kuunga mkono utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli.
Kwa mujibu wa gazeti hilo hadi sasa imebainika kuwa Mkoa wa Arusha ndio unaongoza kwa idadi kubwa ya kata zake kuondokewa na madiwani, huku Halmashauri ya Monduli pekee madiwani wake wanane walijiuzulu na kujiunga CCM.