Rapa kutoka Weusi anayetamba kwa sasa na 'hit song' ya 'Simwachii Mungu', Joh Makini amefunguka na kudai sababu kubwa ya yeye kubadilisha aina ya uimbaji katika muziki ni kutaka kukimbizana na kizazi cha sasa jinsi kilivyo nasio kubakia pale pale alivyokuwa awali.
Joh Makini ameeleza hayo wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha FRIDAY NIGHT LIVE 'FNL' kinayorushwa na tinga namba moja kwa vijana EATV, baada ya watu wengi kumlalamika juu ya uimbaji wake wa sasa hawauelewi na badala wanautaka ule wa awali alioanza nao, licha ya wengine kuwa wanaupenda.
"Huwa nafurahi sana mimi mtu akiniambia ame-miss Joh Makini wa zamani licha ya kuwa nashindwa namna ya kumsaidia kwasababu najiona mimi ni yule yule. Kinachobadilika ni maisha ya watu, floo ya wimbo, mashairi na midundo", amesema Joh Makini.
Aidha, Joh Makini amedai suala la kubadilika ni jambo la kawaida kwa madai anachofanya yeye ni kutaka kukimbizana na nyakati zilizopo nasio vinginevyo.
"Watu waliokuwa wanasikiliza muziki mwaka 2005, vijana kipindi hicho katika mwaka huu wengi wao sio vijana kwa hiyo ili kusudi uendane na generation na wakati uliopo lazima ubadilike, maana huwezi kuzuia mabadiliko, namba zenyewe zinabadilika, watu wenyewe wanakuwa na kubadilika, maisha yanabadilika 'why not me", amehoji Joh Makini.
Kwa upande mwingine, Joh Makini amedai marapa wasasa wanaochipukia wamekuwa wenye bahati nzuri kutokana na uwepo wa mitandao, jambo ambalo linawasaidia katika kutangaza kazi zao bila ya kusuburia 'media' mbalimbali.