Kamati Kuu ya Chadema Kukutana Leo

Kamati Kuu ya Chadema Kukutana Leo
KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inakutana leo jijini Dar es Salaam kujadili mambo muhimu ikiwamo kufanya tathmini ya uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumapili iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, kamati hiyo inakutana kujadili masuala mbalimbali muhimu kuhusu chama hicho na taifa.

Katika taarifa hiyo, Makene alisema miongoni mwa mambo makuu yatakayojadiliwa katika kikao hicho leo ni kupokea taarifa na kujadili juu ya uchaguzi wa marudio wa ubunge, udiwani na hali ya siasa nchini.

"Kikao kitafanyika jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe, kitajikita katika masuala mawili, kupokea taarifa na kujadili kwa kina juu ya uchaguzi wa marudio wa ubunge na udiwani na hali ya siasa nchini," alisema Makene katika taarifa hiyo na kuongeza:

"Wanachama wa Chadema na umma wa Watanzania kwa ujumla utataarifiwa kuhusu maazimio baada ya kikao hicho."

Mbali na wabunge na madiwani kujiuzulu na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimefanya vibaya katika uchaguzi wa Jumapili kwa kulipoteza kwa wapinzani wao hao Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma.

Uchaguzi wa marudio umefanyika katika jimbo hilo kutokana na kufariki dunia kwa aliyekuwa mbunge wake, Kasuku Bilago (Chadema).
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad