Kamishna Mkuu TRA Aagiza Ukaguzi Saa 24 Mipakani

Kamishna Mkuu TRA Aagiza Ukaguzi Saa 24 Mipakani
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Charles Kichere, ameagiza maofisa wake kufanya ukaguzi wa saa 24 katika maeneo yote ya mpakani ili kutokomeza biashara ya magendo.

Vilevile, amesema chombo chochote cha moto kitakachohusishwa na ubebaji wa bidhaa za magendo kitataifishwa kwa mujibu wa sheria.

Kichere alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na maofisa kutoka TRA, Uhamiaji, Jeshi la Polisi na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alipotembelea mipaka ya Tarakea, Rombo na Holili kuangalia utendaji katika mipaka hiyo. 

"Ningependa kuona kila ofisa aliyeko hapa anafanya kazi kwa bidii akijua ya kuwa mapato yanayokusanywa hapa siyo kwa ajili ya TRA tu, ndiyo yanayopelekea kupatikana kwa mishahara ya watumishi wa umma, huduma za afya, shule pamoja na bararaba za kisasa," alisema Kichere.

Aliongeza kuwa kufumbia macho suala la magendo ni kinyume cha maadili na kunaikosesha serikali mapato kwa kuwa bidhaa hizo zinaingizwa bila kulipiwa kodi na kuuzwa kwa bei ya chini na kusababisha bidhaa halali kukosa soko.

"Tuwatumie vyema wananchi wanaoishi mipakani ili wawe mabalozi wazuri wa kulinda kodi zao pamoja na kuwataja wale wote wanaohusika kwa njia moja ama nyingine kupitisha magendo lakini pia tuwe makini kwani baadhi yao wanatumiwa na watu wasio na nia nzuri," alisema.

Kichere pia alitoa wito kwa wananchi wote kutoa taarifa kwa TRA wanapoona watu wanapitisha bidhaa katika njia zisizo rasmi na kuwataka kuwa wazalendo na kutumia bidhaa zinazopatikana nchini.

"Najua kati yenu kuna maofisa ambao siyo waadilifu na ndiyo wanaotumika kutoa taarifa na kushirikiana na wafanyabiashara za magendo, watu hao sitawafumbia macho nitawafukuza kazi na kutaifisha mali zote walizochuma," alisema.

Kichere aliahidi kushirikiana na wakuu wa taasisi zilizopo mpakani kuwachukulia hatua maofisa wote watakaojihusisha au kushirikaina na wafanyabiashara wasio waaminifu wanaokwepa kodi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad