Aika Marealle
SI wageni machoni kwako, masikioni mwako na pengine unawapenda. Wana ‘hit song’ nyingi, zikiwemo Lini, Kamatia, Feel Good na wimbo wao mpya uitwao Fella, unakimbiza mbaya. Kwa upande wa albamu wamefanya mbili, ambazo ni AIM (Above Inna Minute) na Hold Me Back, zaidi wanamiliki studio iitwayo The Industry ambayo ndani yake ina Lebo iitwayo Aika Calvin Marealle.
Nakupa zaidi; Kundi hili ni Waafrika wa kwanza kufanya shoo nchini Israel, na rekodi hii waliiweka baada ya kutoa wimbo uitwao Feel Good, mwaka 2016. Wapo kwenye uhusiano kwa takriban miaka kumi na wamebahatika kupata mtoto mmoja aitwaye Gold aliyezaliwa Desemba, mwaka jana.
Bila shaka ushafahamu ninaowazungumzia, ni Aika Marealle na Emmanuel Mkono wanaounda kundi liitwalo Navy Kenzo. Bila shaka kwa mpenzi wa burudani kuna mengi ungependa kusikia kutoka kwao. Mikito Nusunusu inakusogezea Aika, ana mengi ya kukujuza ambayo pengine huyafahamu kuanzia kwenye kazi zao na ‘life style’ yao, usihamishe ukurasa:
MIKITO: Aika vipi kuhusu mapokezi ya wimbo wenu wa Fella?
AIKA: Kiukweli mapokezi ni mazuri. Wimbo umeenda kiasi cha kufika kwenye ‘platform’ kubwa. Tukizungumzia Uingereza, umesumbua zaidi ya mwezi mzima kwenye chati za muziki za BBC, lakini pia unafanya vizuri Hispania, Russia na Ufaransa. Ni juzi tu tumepewa takwimu kwamba wimbo wetu ni miongoni mwa nyimbo zilizopakuliwa sana kwenye mitandao ya nyimbo Ufaransa.
MIKITO: Mapokezi haya yanawapa picha gani ikiwa mlikaa muda mrefu bila kufanya kazi?
AIKA: Tumegundua kwamba ‘fun base’ yetu inazidi kuongezeka. Watu wanavutiwa na vingi kutoka kwetu. Maisha tunayoishi na mengine mengi. Tumejifunza pia ukiwa na msingi mzuri hata ukikaa miaka miwili ukirudi mashabiki watakupokea tu.
MIKITO: Mnaamini ‘views’ nyingi za YouTube zinatoa picha kwamba wimbo unafanya vizuri?
AIKA: Hapana. Tena kweye hili ninapenda kuwashauri wanamuziki wengine kujiimarisha kwa mashabiki na kuhakikisha kazi zao zinawafikia na pia kwa watu wa ‘media’. Si kila anayetazama wimbo wako YouTube anapenda kazi yako au atapakua muziki wako na kukusapoti.
MIKITO: Kwa sasa Navy Kenzo ni kundi kubwa Afrika, vipi kwa upande wa menejimenti yenu, ipo imara kiasi gani kuhakikisha kwamba mtaendelea kuwa sokoni?
AIKA: Ukiangalia kabla tukiwa wenyewe, yaani Navy Kenzo kama Navy Kenzo chini ya The Industry bado tulikuwa tunafanya vizuri na tumefika mbali. Sasa vipi kwa sasa tulipoungana na Salam Sk na meneja mwingine kutoka Marekani? Hakika ni zaidi ya mwanzo, unaweza kuona picha ya namna tulivyo imara kwa sasa.
MIKITO: Unawezaje kumudu malezi ya mtoto na muziki?
AIKA: Kuna changamoto sana na si jambo rahisi hata kidogo kulea mtoto na kufanya muziki. Tangu tupate mtoto mambo mengi yamekwama kiasi kwamba kuna ‘interview’ nyingi tumezipiga chini ili tu kudili na mtoto. Unajua sisi ni wazazi wapya kwa hiyo mambo mengi tunajifunza.
MIKITO: Watoto wengi wa mastaa wanakuwa na dili nyingi, vipi kwa upande wa Gold?
AIKA: Gold ameanza kupata madili akiwa hata hajazaliwa. Alipata dili kutoka kwenye kampuni iitwalo Kids City Shopping, inayohusiana na vitu mbalimbali kwa mahitaji ya watoto.
Lakini pia ni balozi wa kampuni la mafuta ya nazi iitwayo Africana Products. Kampuni hii inamlipa kila mwezi na kiufupi makampuni haya yote yanampa mahitaji yake mengi.
MIKITO: Malipo ni kama shilingi ngapi hivi?
AIKA: Sitapenda kulizungumzia hilo zaidi.
MIKITO: Unazungumziaje kupata mtoto nje ya ndoa?
AIKA: Kwangu ninaona ni kawaida. Sisi siyo watu wa kwanza kupata nje ya ndoa mtoto, lakini mipango ya kufunga ndoa ipo na muda ukifika tutafunga ndoa.
MIKITO: Una lolote kwa mashabiki wa kazi zenu?
AIKA: Waendelee kutupa sapoti. Hatutawaangusha na tutaendelea kuwapa vitu vizuri