Kauli ya Kubenea Kuhusu kujiunga CCM


MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amefunguka kuhusu taarifa zinazodai yuko mbioni kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Tangu mwaka jana, wimbi la viongozi, wabunge na madiwani wa upinzani kujiuzulu nafasi zao na kujiunga na CCM lilipoanza, Kubenea amekuwa akihusishwa na mpango wa kuihama  Chadema na kujiunga na chama tawala. 

Juzi aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akitetea uamuzi wa viongozi wa upinzani kujiuzulu nafasi zao na kujiunga na CCM. 

Ujumbe huo wa mbunge huyo anayefahamika kwa kutoa habari nyingi za msingi wa makatazo na machukio dhidi ya watu walio mafisadi nchini akiwa mwandishi wa habari, ulisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuibua mjadala kutokana na kuhusishwa kwake kwa muda mrefu kujiunga na chama tawala. 

Ujumbe huo ulisomeka: "Si wote wanaohama wamenunuliwa, ingawa ni kweli kuwa wapo baadhi ya waliohama wamenunuliwa. Kuna wengine wamehama kutokana na kuwapo migogoro, chuki na ubaguzi katika maeneo waliyokuwapo." 

Alipotafutwa na Nipashe jana, Kubenea alikiri kuuandika na kueleza kuwa kuhamia CCM kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, kulimsukuma kuandika ujumbe huo. 

"Ujumbe huo ni kweli ni wa kwangu," Kubenea alisema, "niliandika baada ya Julius Mtatiro kutangaza kuhama CUF na kujiunga na CCM.  

"Inawezekana hakunuliwa, lakini inawezekana njaa ndiyo imempeleka huko kwa sababu kwanza ukumbuke chama chake kina mgogoro mkubwa, pia upande aliokuwa yeye, hakuna ruzuku. Kwa hiyo, hawakuwa na pesa ya kujiendesha na ndiyo maana akaona ahame tu. 

"Nasema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao mimi nawafahamu, walihama na hawakununuliwa isipokuwa walishindwa kuvumilia baada ya kukutana na watu ambao walitofautiana nao kimawazo, yaani mawazo yao yalikinzana, wao badala ya kuvumilia walishindwa." 

KUHAMIA CCMAlipoulizwa na Nipashe kuhusu kama naye ni miongoni mwa wanaodaiwa wako kwenye foleni ya kujiunga na CCM, Kubenea alisema hana mpango wa kukihama chama chake kwa sasa. 

"Mimi sina kabisa mpango wa kuhama chama changu (Chadema), hicho nilichoandika yalikuwa ni maoni yangu tu baada ya Mtatiro kuhama na si vinginevyo, watu wasahau kabisa na wasifikirie kwamba mimi naweza kuhama," Kubenea alisema na kueleza zaidi: 

"Unajua vyama vya siasa siyo madhehebu ya dini, misikiti au makanisa kusema watu wasipishane mitazamo, vyama vyote vya siasa watu wanapishana mawazo na mitazamo. 

"Na hiyo sioni kama ni sababu kubwa ya kukufanya eti uhame, kwani huko unakokwenda wenyewe hawatofautiani? Mbona kila chama watu wanatofautiana?" 

Kubenea alichaguliwa kuwa Mbunge wa Ubungo baada ya kushinda uchaguzi wa Oktoba 25, 2015. Ni mmiliki na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd na katika kutekeleza majukumu yake ya uandishi wa habari, alifahamika kwa kuandika habari za kufichua ufisadi. 

Januari 5, 2008, alivamiwa ofisini kwake na kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana na kulazimika kupelekwa India kwa matibabu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad