Kelvin John "Siwazii Kucheza Timu za Bongo, Nataka Kuwa Kama Mbwana Samatta"


KELVIN John, yule straika matata wa Timu ya Soka ya Vijana ya Taifa U-17 ‘Serengeti Boys, amesema wala haiwazii Ligi Kuu Bara, bali anachokitamani ni kucheza katika moja ya ligi za Ulaya kisha timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars.

John alisema anataka kuwa kama Mbwana Samatta anayekipiga Ligi Kuu Ubelgiji au mastaa wengine wa Bongo kina Simon Msuva aliyeko Morocco na Abdi Banda aliye Afrika Kusini.

Straika huyo ambaye kabla ya mechi ya jana Ijumaa dhidi ya Uganda alikuwa anaongoza kwa ufungaji akiwa na mabao sita dhidi ya matano ya Mganda, Ssekajja Davis alisema anafahamu kufikia malengo hayo si kazi nyepesi, bila kuwepo na juhudi binafsi, nidhamu na kuzingatia kile anachofundishwa na kocha wake.

“Kuna wachezaji wanaoonekana kuwa tegemeo ndani ya Taifa Stars, naamini mpaka wanaaminiwa hivyo, lazima watakuwa wana nidhamu na kujitambua wao ni kina nani, ndivyo nataka iwe kwangu,” alisema Kelvin ambaye moja ya mabao yake alilofunga dhidi ya Rwanda lilikuwa gumzo.

Bao hilo lililokuwa la kwanza kati ya matatu aliyoyafunga akichangia ushindi wa 4-0, alitoka katikati ya uwanja na mpira kisha kuwalamba chenga mabeki wote na kipa pia kabla ya kutupia wavuni.

John alisema atajitahidi kufanya makubwa katika michuano hiyo ya vijana wa umri wake na pia kwenye fainali zenyewe zitakazochezwa mwakani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad