Akiwaeleza waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, kuhusu yaliyozungumzwa katika kikao kati ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe na wadau na wamiliki wa televisheni nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa serikali imefikia uamuzi huo baada ya visimbuzi vya AZAM, ZUKU na DSTV kutoonesha channeli za ndani, kulingana na aina ya leseni zao.
“Ningependa watanzania wafahamu kwamba kuanzia septemba 5 mwaka huu, visimbuzi vya Ting, Starmedia, Continental na Digtek vitaonesha takribani channeli 34 za ndani bure, ili kutoa fursa ya kila mwananchi kuwa na haki ya kupata taarifa” alisema Dkt. Abbasi
Aidha, alielezea kuwa wadau hao na wamiliki wa televisheni wameonesha kuridhishwa na hatua hiyo kwa vile Serikali imetengeneza miundombinu itayoruhusu channeli zao kuonekana nchi nzima.
Dkt. Abbasi, alisisitiza kuwa “nchi imeandaa mfumo, ambao unaweza kufanyakazi bila kutegemea kampuni kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuonesha channeli za ndani au matangazo, kwa hivyo wadau au wamiliki wa vyombo vya habari wasihofu kuhusu hilo”
Kikao kati ya Waziri Mwakyembe na wadau na wamiliki wa televisheni nchini, kimefanyika kwa lengo la kuwa na majadiliano ya pamoja baina serikali na wadau hao ili kupata muafaka kuhusu kutooneshwa kwa chaneli za ndani katika visimbuzi vilivyokiuka masharti ya leseni zao.
Aidha, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Injinia James Kilaba, pamoja na wataalamu wake.