Waziri wa Nishati Medard Kalemani amewapa siku 14 wakuu wa taasisi na vitengo vyote vinavyoshiriki utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwenye maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers Gorge) kuwasilisha taarifa ya mpango kazi ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumza jana Agosti 3 mara baada ya kutembelea eneo la mradi huo unaotarajia kuzalisha umeme wa megawati 2100, Profesa Kalemani amesema taarifa za mpango kazi huo ziwasilishwe kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati.
Pia Kalemani aliwataka wakuu hao wa vitengo na taasisi kuimarisha mawasiliano na usimamizi wa kazi na kwamba lazima mradi huo ukamilike kwa wakati.
“Nataka uharakishaji wa manunuzi ingawa kuna sheria za manunuzi lakini hicho kisiwe kigezo cha kuchelewesha mradi,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameahidi wizara yake itaharakisha kufanya tathmini ya mali, nyumba na hoteli zinazotakiwa kuondolewa ili kupisha mradi huo.
“Nitasimamia ufanyikaji wa tathmini hiyo na kutoa notisi kwa mujibu wa sheria kwa wamiliki wa mali hizo,” amesema.
Pia amesema kuwa wizara kupitia wataalamu wake watapima eneo lote la mradi na vijiji viwili na kupangiwa matumizi bora ya ardhi.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kampuni tanzu ya Tanesco –ETDCO Elangwa Abubakar aliiomba wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza idadi ya askari watakaolinda wakati wa kazi ya utandazaji wa nyaya za umeme utakaopelekwa kwenye eneo la mradi.
Amesema askari waliopo hawatoshi hasa ukizingatia eneo la mradi liko ndani ya hifadhi ambapo kuna wanyama wakali hivyo aliiomba wizara hiyo iongeze askari 24 katika eneo hilo.
Kutokana na ombi hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema kuwa wizara hiyo itafanikisha upatikanaji wa askari hao isipokuwa kila kitengo kiainishe muda na kazi itakayofanyika.