Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amemjia juu mbunge wa zamani wa Monduli, Julius Kalanga akidai kwamba amesema, “Nimemtanguliza Ikulu.”
Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa Monduli hadi mwaka 2015 alipojiunga na Chadema na kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho akiungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, alisema pia kwamba kuna madai yanayosambaa kwamba yupo mbioni kuwatoa wabunge na madiwani wa Chadema na kuwapeleka CCM.
“Wanasema kazi hiyo nimeivalia njuga na ninaifanya vizuri sana na kwamba tumekubaliana na Rais (John) Magufuli nimfanyie kazi hii. Waongo wakubwa hao, tena wamesema Mto wa Mbu, wamesema Monduli na kwenye magazeti kadhaa na kwenye mablog lakini nataka niwaeleze kwamba ni waongo wakubwa hao,” alisema waziri mkuu huyo wa zamani huko Migungani, Arusha hivi karibuni.
Alisema, “Kwa hiyo nimesimama kusema sijamtuma mtu yeyote kwa Rais na sina mpango wa kufanya hivyo, acheni kumsingizia Rais acheni kunisingizia ugomvi kati ya Rais na mimi, sina ugomvi na Rais Magufuli.”
Aidha, Lowassa alisisitiza, “Kuna mashindano ya kuhama vyama, wanafanya nchi nzima, wanaohama nawatakia kila la heri. Lakini wasitafute mchawi, waseme naenda kwa hoja zangu hizi hizi, sio kwa sababu fulani amenitanguliza.”
“Aliyekuwa mbunge wa Monduli (Julius Kalanga) alisema hadharani amenitanguliza Ikulu, huo ni uongo wa kutupwa… kwa hiyo mimi sina miguu? Kama nataka kwenda si nitakwenda kwa miguu yangu, eti anasema nimemtuma nimemtanguliza kwenda Ikulu, watu wa Monduli wote watahamia chama chake.
“Anasema uongo kwenye kinywa chake, lakini nasema huhitaji kuomba ruhusa kuhama chama, hiari yako mwenyewe.”
Hata hivyo, jana alipoulizwa kuhusu madai hayo, Kalanga ambaye baada ya kuhamia CCM ameteuliwa na chama hicho kuwania tena nafasi hiyo amekanusha kusema hayo akisisitiza kwamba hajawasiliana na Lowassa kwa muda mrefu.
Kuhusu wanasiasa kuhama vyama, Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema, “Ndugu zangu wala msitishike, kuhama vyama ni utaratibu wa kisiasa ndiyo mchezo wa wanasiasa. Raila Odinga amehama vyama mara saba.”
Alitoa mfano wa Nigeria akisema kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, tayari kuna wanasiasa karibu 400 kwenye Bunge kubwa la nchi hiyo na zaidi ya 200 kwa Bunge la kawaida ambao wamehamia vyama vingine.
“Wanahama usiku na mchana, ukisikia mtu anahama funika blanketi lako... ana hoja zake na sababu zake na nyingi ni za uongo. Zile za kweli utakutana na wenzako mbele ya safari. Sasa usisingizie watu. Amesingizia mbunge wa Monduli kwamba anakwenda kwa sababu hakuna maendeleo anayoweza kufanya, mwongo.”
“Nimekaa Monduli miaka tuliyokaa tumefanya maendeleo, hatukufanya? Akajibiwa na wananchi, “tumefanyaaaa.” Akaendelea, “Tuna shule ya sekondari katika kila kata, tunazo hatunazo?” Akajibiwa, “Tunazoooo.” Akaendelea kuhoji, “Tunayo hospitali ya wilaya, tunayo hatunayo? Akajibiwa, “Tunayoooo.” Mwisho akauliza, “Tuna barabara ya lami, tunayo hatunayo? Akaambiwa “Tunayoooo”. Kisha akahoji, “Mungu atupe nini?”
Kalanga aruka
Licha ya kukanusha kutoa maneno hayo, Kalanga alisema, “Nina miezi zaidi ya sita sijaonana na Lowassa. Hizi taarifa ambazo nimemsikia akinituhumu Mzee Lowassa nadhani watu wake wamempotosha.”
Kalanga alisema anamheshimu Lowassa na asingependa malumbano naye.
Kabla ya kujiunga na Chadema mwaka 2015, Kalanga alikuwa diwani wa Lepurko na mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Wilaya ya Monduli, huku Lowassa akiwa mbunge wake.