Lugola Atoa Amri kwa Polisi Kuwakamata Wanafunzi Watoro

Lugola Atoa Amri kwa Polisi Kuwakamata Wanafunzi Watoro
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewapa wiki moja Jeshi la Polisi Wilaya Bunda, kuwakamata wanafunzi watoro, wazazi wa wanafunzi watoro pamoja na watu waliowarubuni wanafunzi wa kike ambao wameacha shule wilayani humo.

Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, alisema inamsikitisha sana idadi kubwa ya wanafunzi wilayani humo wameacha masomo yao na kurubuniwa wanaume ili waweze  kuolewa huku Serikali ikitangaza elimu bure kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha nne.

Akizungumza na mamia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa mpira wa miguu wa Busambara, Kijiji cha Busambara, Kata ya Kitengule, wilayani humo, Lugola alisema kiwango cha wanafunzi kuacha masomo inatisha, hivyo serikali haiwezi kukaa kimya, lazima kuhakikisha wanafunzi hao wanasoma ili waje kuwa viongozi wa nchi.

“Mkuu wa Polisi wa hapa Bunda, nawapa wiki moja, mtumie elimu zenu za upelelezi mliofundishwa, wakamateni, wachunguzeni, wahojini ndugu,  jamaa, majirani mtawawapata wote wanaowarubuni watoto hawa, halafu mushughulike nao,” alisema Lugola.

Pia Lugola aliongeza kua,  kuna sheria zinazoshughulika na wanafunzi watoro na pia zipo sheria zinazoshughulika na wazazi wa wanafunzi watoro, pia zipo sheria zinazowashughulikia wanaume wanaowarubuni wanafunzi, hivyo haiwezekani wanafunzi wa kidato cha tano wakatae masomo, na wengi wao wanaokataa masomo ni wasichana.

Aidha, Lugola alisema ujenzi wa sekondari mbili za kidato cha tano na sita unaendelea ambapo katika kata za Nansimo na Muramba katika Jimbo lake la Mwibara zitanaanza kuchukua wanafunzi mwaka ujao watakao fanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.

“Tunaendelea kuweka miundombinu katika shule hizo ili ziweze kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano katika maeneo haya na hatutarajii wanafunzi kukosa shule wamalizapo kidato cha nne,” alisema Lugola.

Hata hivyo, Lugola pia aliwataka polisi nchini kuwakamata waendesha magari na bodaboda ambao hawafuati sheria za barabarani ikiwemo baadhi ya bodaboda uvunja sheria kwa makusudi kwa kupakia abiria wanne na kuendelea ambapo ni hatari kwa usalama wa dereva na abiria hao.

“Idadi kubwa ya polisi wanafanyakazi kwa umakini na uaminifu mkubwa, ila wachache sana ndio wenye tabia hizo mbaya, nawataka askari hao wafuate sheria na pia kuendelea kuzikamata kama ni magari au bodaboda au wananchi wowote ambao wanavunja sheria za nchi,” alisema Lugola.

 Waziri Lugola yupo katika ziara jimboni kwake kwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwaunganisha wananchi kupitia Bonanza lake la michezo ya mpira wa miguu ambalo linashirikisha kila kata wakitoa washindi mbalimbali ambao anawapa zawadi pamoja na kuingia moja kwa moja katika mashindano ya kugombea Kombe la Kangi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad