Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola amewaonya wakuu wa mikoa na wilaya kutotumia vibaya sheria na kuwaweka ndani wananchi. Amesema Serikali ya Awamu ya Tano haitakubali wananchi wanyanyaswe.
Agosti 14, 2018 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alikemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo kuwaweka watu ndani.
Aliwataka wakuu hao wa wilaya kuhakikisha wanasoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ili kufanya kazi kwa weledi.
Katika siku za karibuni, wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia ‘sheria ya saa 48’ kutoa adhabu kwa kuwaweka baadhi ya watu mahabusu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Agosti 28, 2018 Lugola mbali na kuwaonya wakuu hao wa mikoa na wilaya, pia aliwashukia askari polisi wanaolichafua jeshi hilo kwa kuwabambikia kesi wananchi.
“Hayo mambo yako kisheria na hiyo sheria ina vigezo vyake na kama vimetimia, watakuweka ndani. Kama DC ameona huyu tusipomweka ndani usalama wake utakuwa hatarini, lazima atakuweka,” amesema.
“Lakini siyo mtu yuko kwenye mkutano ameuliza swali ambalo DC anaona linaleta challenge (changamoto), anasema huyo weka ndani saa 48. Hilo halitawezekana, katika Serikali hii hatutaki wananchi wapate shida.”