Lugola Kula Sahani Moja na Polisi Wala Rushwa

Lugola Kula Sahani Moja na Polisi Wala Rushwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema hatawaonea huruma polisi watakaokamatwa wakichukua rushwa na wale wanaonyanyasa wenye magari, bodaboda na wananchi.

Lugola ambaye ni mbunge wa Mwibara, alisema anapokea taarifa mbalimbali zikilalamikia tabia za baadhi ya polisi kuwaonea wananchi wasio na makosa kwa kutumia nguvu na kuwalazimisha kuwaweka mahabusu hata kama kosa halistahili kuwekwa ndani.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Victoria, Mji mdogo wa Kisorya, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, jana, Lugola alisema atahakikisha anapambana na askari ambao wamechoka kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

“Serikali ya awamu ya tano si ya mchezo mchezo, nawahakikishia wananchi wa hapa Kata ya Nansimo na pamoja na kote nchini, mimi Lugola sitamwangusha mheshimwa Rais Magufuli, sitawaangusha nyie wananchi, ninawaahidi hii tabia nawahakikishia kwa mara nyingine nitaimaliza,” alisema Lugola huku akishangiliwa.

Aliongeza kuwa magari na bodaboda ambazo hazina makosa, hazipaswi kubughudhiwa kwa sababu wamefuata taratibu zote za usalama barabarani.

“Kitendo cha askari akiwa na masilahi yake binafsi au ametumwa na mtu mwenye masilahi naye kwenda kukamata gari fulani au bodaboda kwa lengo la kujipatia rushwa tabia hiyo inapaswa kulaaniwa.

“Muda mwingine utakuta mwananchi mmoja ambaye ana masilahi na polisi anakamata gari au bodaboda yake na mmiliki wa chombo hicho cha moto huwekwa mahabusu na ukiuliza ‘nimefanya kosa gani’ wanakujibu ‘kaa ndani kwanza’, na ukiingia bure, lakini wanapokutoa unawapa rushwa, nalijua hilo vizuri sana, tabia hii haivumiliki, na nitahakikisha wananchi wa jimbo hili pamoja na Tanzania nzima mtakuwa salama,” alisema Lugola.

Alifafanua kuwa kuna baadhi ya polisi huwaweka mahabusu wananchi hovyo ili kuwatisha kwa lengo la kujipatia rushwa.

“Si kila kosa mwananchi awekwe mahabusu, yapo makosa ambayo polisi wanaweka mahabusu wananchi kwa mujibu wa sheria, lakini kitendo cha askari kumkamata mwendesha bodaboda akimlazimisha atoe rushwa au awekwe mahabusu hilo halitakubalika,” alisema.

Pia alisema wananchi wanapoonewa mara kwa mara kunatengeneza chuki dhidi ya Serikali, kwa sababu wanastahili kuishi katika mazingira ya amani na utulivu, hivyo tabia ya baadhi ya askari hao haiwezi kuvumilika.

“Hii tabia ya baadhi ya askari wanasema ‘injika ugali mke wangu mboga inakuja’ akielekea barabarani au mahali popote na kuanza kutafuta rushwa kwa nguvu zote kwa wenye magari, bodaboda au mazingira yoyote.

“Mimi Kangi Lugola naapa nitaisambaratisha haraka iwezekanavyo tabia hii, sitakuwa na huruma katika hilo na nitakuwa nafanya ziara ya kushtukiza ili niwakamate hao wenye tabia hiyo chafu katika nchi yetu,” alisema Lugola.

Hata hivyo, Lugola aliwataka polisi nchini kuwakamata waendesha magari na bodaboda ambao hawafuati sheria za barabarani.

Alitoa mfano baadhi ya waendesha bodaboda wanaovunja sheria kwa makusudi kwa kupakia abiria zaidi ya wane, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa dereva na abiria wake.

“Polisi wangu wengi wanafanya kazi kwa umakini na uaminifu mkubwa, ila wachache sana ndio wenye tabia hizo mbaya, nawataka askari hao wafuate sheria na pia kuendelea kuzikamata kama ni magari au bodaboda au wananchi wowote ambao wanavunja sheria za nchi,” alisema Lugola.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad