Mahakama Yaamuru Mwili Uliosuswa na Ndugu Uzikwe

Mahakama yaamuru mwili uliosuswa na ndugu uzikwe
Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya imeamuru mwili wa Frank Kapange wa jijini Mbeya kuzikwa na ndugu zake, baada ya kutupilia mbali maombi ya familia ya kutaka polisi ifanye uchunguzi wa kiini cha kifo chake.

Frank alifariki Juni 4 mwaka huu na mwili wake kuhifadhiwa mochwari katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Taarifa za uongozi wa hospitali hiyo zinaeleza kuwa mwili huo ulipelekwa na polisi na hadi leo unatimiza siku 78 ukiwa mochwari.

Familia ya Frank ilisusa mwili huo na kufungua kesi mahakamani wakiomba ufanyike uchunguzi wakidai alifariki mikononi mwa polisi.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliandika mapingamizi ya shauri hilo hivyo kuitaka mahakama hiyo kutupilia mbali kwa madai kwamba maombi yaliyowasilishwa na walalamikaji yalikosewa kisheria.

Akisoma uamuzi huo mdogo leo Agosti 24, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite amesema mahakama yake imejiridhisha kwa hoja kuu mbili za kutupilia mbali shauri hilo baada ya hoja ya mawakili upande wa Jamhuri.

Mteite amesema hoja ya kwanza ni kuwa hati ya kiapo ilikosewa.

“Badala ya kutengenezwa na mlalamikaji lakini wakili wa utetezi ndiye aliyetengeneza kana kwamba ndiyo mlalamikaji kitu ambacho ni kosa lakini pia uthibitisho wa kiapo hicho haukukamilika kisheria,” amesema.

Hivyo mahakama ikawataka mawakili hao kujibizana hoja hizo kwa maandishi na upande wa Jamhuri ukafanya hivyo na upande wa utetezi ulipaswa kujibu hoja zake kupinga mapingamizi ya Jamhuri ndani ya siku 14 kitu ambacho wakili wa utetezi hakukifanya.

“Kutokana na sababu hizo na wakili wa utetezi kutoonyesha umakini wa suala hilo na kwa kuzingatia tamaduni za kiafrika mtu akishafariki anapaswa kusitiriwa mapema iwezekanavyo ili kuwapunguzia machungu ndugu na familia,” amesema.

Amesema mahakama inakubaliana na hoja za upande wa Jamhuri na kuamuru mwili huo kuzikwa.

“Kwa maana hiyo, mahakama hii inamuelekeza Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya kuutoa mwili huo kwa ndugu ili wakauzike na familia hiyo kama haitauchukua mwili huo basi mahakama hii pia inamtaka mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na uongozi wa jiji la Mbeya kwenda kuuzika mwili huo,” amesema Hakimu Mteite.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad