Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, Songwe imemuachia huru mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga na wenzake wawili baada ya kukutwa hawana hatia katika kesi iliyokuwa ikiwakabili.
Haonga na wenzake, Wilfredy Mwalusamba (katibu wake) na Mashaka Mwampashi wameachiwa huru leo mchana Ijumaa Agosti 10, 2018.
Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kufanya fujo na kuvuruga mkutano wa uchaguzi wa baraza la mji mdogo wa Mlowo, kosa la pili na tatu ni kuwazuia askari kutekeleza majukumu yao.
Akisoma huku hiyo leo hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Nemes Chami amesema katika mashtaka yote matatu, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha makosa.
"Katika ushihidi wa mashahidi sita wa upande wa Jamhuri hakuna mahali walipothibitisha kwamba washtakiwa walikataa kukamatwa,” amesema.
“Hakuna mahali walipoonesha kwamba washtakiwa hawa waliwazuia askari kutekeleza majukumu yao na hakuna mahali walipothibitisha kwamba washtakiwa walilazimisha kurudi ukumbini baada ya kutolewa nje.”
Amesema kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha ushahidi wa mashtaka waliyoyawasilisha mahakamani hapo, mahakama inawaachiria huru washtakiwa wote.
Amesema kama kuna upande unaona haujaridhika na hukumu hiyo una haki ya kukataa rufaa ndani ya muda wa kisheria.