Makamu wa Rais na Mbabe wa Zamani wa Kivita Azuiwa Kuwania Urais DRC

Makamu wa rais na mbabe wa zamani wa kivita azuiwa kuwania urais DRC
Mbabe wa zamani wa kivita Jean-Pierre Bemba hawezi kuwania urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, tume ya uchaguzi nchini humo imesema.

Bw Bemba ni miongoni mwa wagombea sita waliokuwa wamewasilisha majina yao kutaka kugombea, lakini tume hiyo imesema hawajahitimu baada ya mashauriano ya saa kadha.

Kiongozi huyo wa zamani wa waasi aliachiliwa huru baada ya mahakama kubatilisha hukumu dhidi yake ya kumpata na hatia ya uhalifu wa kivita mwezi Juni.

Tume ya uchaguzi imesema Bw Bemba amezuiwa kuwania kwa sababu alipatikana na hatia ya kuwahonga mashahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).

Bw Bemba, aliyerejea DR Congo mwanzoni mwa Agosti baada ya kukaa miaka 11 uhamishoni au gerezani, amewasilisha rufaa kupinga hukumu hiyo dhidi yake katika ICC.

Uchaguzi wa mwaka huu utafanikisha kuchaguliwa kwa mrithi wa Rais Joseph Kabila, ambaye muhula wake wa pili na wa mwisho wa kuongoza ulimalizika miaka miwili iliyopita.

Muungano tawala nchini humo ulimteua waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary kuwa mgombea wake.

Kulikuwa na jumla ya watu 25 waliotaka kuwania, wakiwemo mawaziri wakuu wa zamani Antoine Gizenga na Adolphe Muzito. Wawili hao pia wamekataliwa kuwania.

Vyama vya upinzani vilishutumu hatua hiyo ya tume ya uchaguzi hata kabla ya uamuzi huo kutangazwa rasmi, wakiituhumu serikali ya sasa kwa kujaribu kudhibiti na kuelekeza mchakato wa uchaguzi.

Wale waliozuiwa kuwania, akiwemo Bw Bemba anayetazamwa na wengi kama mgombea anayetoa ushindani mkali zaidi kwa muungano tawala wa Bw Kabila, wanaweza kukata rufaa uamuzi huo wa tume.

Orodha kamili na ya mwisho ya wagombea inatarajiwa kuchapishwa mwezi Septemba.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad