Mnada wa pili wa makontena 20 yenye samani zikiwamo meza na viti, yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, utafanyika Septemba Mosi baada ya ule wa Agosti 25 kutofanikiwa kupata wanunuzi.
Makontena hayo ambayo yamekwama bandarini yanadaiwa kodi ya Sh bilioni 1.2.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa (TRA), Richard Kayombo, amesema mamlaka hiyo imeazimia kufanya mnada wa pili Jumamosi ya wiki hii.
Alisema mnada huo utaanza saa 2:00 asubuhi kwa kufuata taratibu zote za sheria kama mnada wa awali ulivyofanyika, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa ajili ya kununua samani hizo kwa kufuata taratibu na sheria za minada.
Alisema TRA haiwezi kutangaza bei ya mnada huo kabla ya kufanyika kwa sababu ni siri, lakini wateja watakaofika watakuta bei ambayo imepangwa kwa mujibu wa sheria serikali iweze kupata mapato yake.
Aliwaomba wananchi kuondoa hofu kuhusu samani hizo na kuwataka kujitokeza waweze kununua samani hizo.
Baada ya mnada wa Agosti 25 kukwama kwa wateja kushindwa kufikia bei iliyotangazwa, Makonda alijitokeza na kusema mtu atakayenunua makontena hayo aliyosema yana samani za shule za Dar es Salaam, atalaaniwa na Mungu.
Baada ya kauli hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alimjibu Makonda akisema makontena hayo yatapigwa mnada mteja atakapopatikana na wala hatishiki na laana zozote.