SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) kupitia kwa Ofisa Mashindano, Baraka Kizuguto limethibitisha kuwa maandalizi kuelea mchezo wa Ngao ya Hisani baina ya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar yamekamilika kwa asilimia kubwa.
TFF imeomba mashabiki wa soka jijini hapa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM kirumba jijini hapa.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kizuguto amesema: “Maandalizi yamekamilika, TFF kwa kushirikiana na serikali ya Mkoa wa Mwanza tumejipanga vizuri, viingilio katika mchezo huo itakuwa shilingi 10,000 kwa VIP, Sh 5,000 kwa mzunguko lakini pia watoto nao wataweza kuingia kwa kiingilio cha shilingi 1,000.
“Tiketi zitauzwa siku ya mchezo ambapo milango nane itakuwa wazi kwa ajili ya uuzwaji wa tiketi hizo, hivyo tunaamini kwamba mashabiki wa soka watajitokeza kwa wingi katika mchezo huo.”
Katika hatua nyingine Kizuguto amesema kuanzia jana Alhamisi timu zilianza kuingia Mwanza na tayari mamlaka zinazohusika zimethibitisha kujaza askari kwa wingi uwanjani lengo ni kuhakikisha kuwa mtu atakapofika uwanjani anakuwa salama.
Aidha, Kizuguto alisema leo Ijumaa kunatarajiwa kuwa na kongamano la soka litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Gold Crest jijini hapa.