Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limeongeza mapato yake ya kila mwezi hadi kufikia Sh4.5bilioni kuanzia mwaka 2017, ikiwa ni tofauti na mwaka 2016 ambako ilikuwa ikikusanya Sh700milioni kwa kila mwezi.
Kiwango cha hasara katika shirika hilo ambalo lilianza kufufuliwa mwishoni mwa mwaka 2016, nacho kimepungua kutoka Sh14.2 billioni mwaka 2016 hadi Sh4.3 bilioni mwaka 2017 huku ukubwa wao wa soko katika usafirishaji wa anga nchini ukiwa ni asilimia 24.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Agosti 13, 2018 na kaimu meneja wa mauzo na usambazaji wa shirika hilo, Edward Nkwabi katika mkutano na mawakala wa tiketi za ndege uliofanyika jijini hapa.
Kampuni hiyo iliwaeleza mawakala mpango wake wa kuimarisha kituo cha huduma kwa wateja na kuongeza safari zake katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi ikiwemo safari mpya ya Entebe-Uganda, Bujumbura- Burundi, Mumbai-India na Guangzhuo- China.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya udalali ya ABC Travel and Tours Limited, Saleh Pamba amehoji kwanini ATCL haianzishi safari kati ya Ulaya na Amerika ambako asilimia 70 ya watalii wote wanaokuja nchini wanatokea huko.
Akijibu swali hilo, mkurugenzi mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema kwa sasa wanajiimarisha kwanza kuweza kuwa washindani katika maeneo hayo, kwamba uwezo wao sasa ni kwenda India na China ambako kuna abiria wengi lakini ushindani ni mdogo.
"Mpango wetu wa biashara unaonyesha kuwa baada ya ujio wa Dreamliner nyingine tutakuwa na Safari ya London. Soko la Amerika na Ulaya ni kubwa kwa kuwa na idadi kubwa ya abiria lakini kuwapata si rahisi kutokana na ushindani uliopo lakini tukishajiimarisha zaidi tutaweza kwenda huko," amesema Matindi.