Mchekeshaji maarufu nchini Tanzania, Masanja Mkandamizaji amedai kuwa kitendo cha mwanaume kuvaa cheni mguuni ( kikuku) hiyo sio dhambi katika Imani ya Kikristo bali ni fasheni tu.
Masanja amesema kuwa Kikuku ni cheni tu ya kawaida ambayo mtu anaweza akaamua kuvaa miguuni, mikononi, shingoni na hata sehemu nyingine yoyote ya mwili wake kuendana na fasheni anayoitaka na wala sio dhambi na hakuna sehemu iliyoandikwa kufanya hivyo ni dhambi.
“Kama mchungaji nasema mwanaume kuvaa kikuu mguuni sio dhambi, lakini nikawaambia kwenye maadili kuvaa kikuku unamaanisha nini? soo shinda ikiwepo kwenye maadili haina maana ni dhambi watu wanadhani kuwa vitu wasivyovipenda wao kuviona, vitu ambavyo sio maadili mazuri wanafikiri kuwa ni dhambi kuna tofauti sana juu ya hivyo vitu. Kwa hiyo narudia tena kusema mwanaume kuvaa kikuku katika Biblia sio dhambi.“amesema Mchungaji Masanja kwenye mahojiano yake na MASANJA TV huku akirejea kitabu cha Kumbu kumbu ya Torati 22:5 .
Hata hivyo, Masanja amesema Cheni ni cheni tu na hakuna mtu wa kumpangia binadamu mwenzie sehemu ya kuvaa na hakuna cheni ya mwanamke zote ni cheni tu.
“Kikuku ni cheni tu, hakuna cheni ya kivulana wala cheni ya kike cheni ni cheni na ukiamua kuvaa mkononi au shingoni sio dhambi kufikiria vibaya mtu kuvaa cheni mguuni huo ni uchizi wa hali ya juu. Kwahiyo kama kuna mtu anaona kuvaa micheni miguuni ndio raha muacheni avae“.
Kwa upande mwingine Masanja amesema kuwa Mungu hajamuumba binadamu aokoke ili awe nyuma ya fasheni bali alimuumba aendane na fasheni pia na amediriki kusema kuwa hata yeye angekuwa vizuri kiuchumi angenunua cheni za dhahabu na kutupia shingoni.
Masanja ametoa kauli hiyo ikiwa ni mwezi mmoja sasa umepita tangu msanii wa muziki nchini Tanzania, Diamond Platnumz avae cheni mguuni wakati akiwa kwenye ziara yake ya kimuziki nchini Marekani jambo ambalo lilizua kwenye mitandao ya kijamii nchini.
Masanja Amtetea Daimond "Mwanaume Kuvaa Kikuku Mguuni ni Fasheni sio Dhambi"
0
August 06, 2018
Tags