Wamevuana nguo! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Shehe Juma Ahmed Kikwesa, mkazi wa Lugala mkoani Morogoro kumtuhumu Shehe Ahmadi Said Khairallah kuwa anamtongoza mkewe aitwaye Rehema Said.
Tukio hilo lililofuatiliwa kwa undani na Mtandao huu, limedaiwa kutokea Mei, mwaka huu mwezi ambao waumini wa dini ya Kiislamu walipokuwa kwenye mfungo mtukufu wa Ramadhan hivyo kuibua gumzo katika mitaa mbalimbali.
Sakata hilo la viongozi hao wakubwa wa dini kushindwa kumalizwa kimyakimya hadi kuwafikia waumini, liliwafanya waumini wengi wapigwe na butwaa huku wengine wakiona aibu kukutana nao maana wanawaheshimu.
“Yani sijui jamani imekuwaje wameshindwa kuyamaliza kwa siri hadi sisi waumini tumeyajua, mimi binafsi naona hata aibu kukutana nao,” alinukuliwa mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa chanzo, Shehe Khairallah ambaye ni Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) Mkoa wa Morogoro, alianza kitambo kumtaka mke wa Shehe Juma ambaye ni Imamu Msaidizi wa Msikiti wa Lugala huku katibu huyo akiwa ndiye aliyefungisha ndoa ya Juma.
“Iko hivi, Juma na Shehe Khairallah ni majirani na marafiki wa karibu kwani wote wanakaa Lugala. Khairallah ndiye aliyefungisha ndoa ya Juma mwaka 2005. Baada ya kuwafungisha ndoa, kuanzia mwaka 2011 hadi 2013 Shehe Khairallah alianza kumchombeza mke wa Juma lakini ilipofika mwaka 2013 akaacha,” kilisema chanzo hicho makini.
Kikizidi kuelezea sakata hilo, chanzo hicho kilidai kuwa, ilipofika mwaka 2018, Shehe Khairallah akaanza tena ‘kumuimbisha’ na ndipo Juma alipomueleza mkewe wakusanye ushahidi na kumshtaki katika Baraza la Mashekh wa Wilaya Mtandao huu unayo nakala ya shauri hilo).
“Ilikuwa ni mwezi wa Ramadhan (Mei mwaka huu), sasa mke wa Juma alipokuwa anakusanya ushahidi wake, alimrekodi Shehe Khairallah alipokuwa akimtongoza, akaweka ushahidi wa miamala ya pesa aliyomtumia pamoja ndipo wakapeleka ushahidi huo katika baraza la mashekh wa wilaya.
“Jopo la mashehe wa wilaya lililoongozwa na Shehe wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Abdulrahaman Shaban Kiswabi na mashehe wengine wanne; Mohamed Salim Masenga, Mussa Bolingo, Ramadhan Rashid na Therey Jafaar walisikiliza shauri hilo na kutoa hukumu,” kilisema chanzo hicho.
Kabla ya kutoa hukumu, chanzo hicho kilieleza kuwa, mshtakiwa aliitwa na kupewa nafasi ya kujitetea ambapo aliomba mke wa mshtaki afike ili kutoa ushahidi wake.
Hata hivyo mke wa mshtaki alipofika na kutoa maelezo yaliyoshibisha madai ya mumewe, awali mshtakiwa aliikana sauti iliyotolewa kama ushahidi na kusema si yake lakini baadaye alikiri kuwa ni yake na kusema alikuwa anazungumza na mwanamke huyo ili kuangalia uwezekano wa kumuoa kwani alimueleza kuwa ameachana na mumewe.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, baraza hilo lilimtia hatiani Shehe Khairallah kwa kosa la kuvuruga ndoa ya muislamu mwenzake (Juma) na kumhukumu hukumu ya onyo; kosa lisilo na adhabu wala fidia. Baraza hilo pia lilimuandikia barua Shehe Mkuu wa Mkoa, Twaha Saleh Kilako ili aweze kuamua hatma ya nafasi ya Shehe Khairallah kama Katibu wa Bakwata Mkoa.
Katika barua hiyo ya jopo la mashehe wa wilaya, waliambatanisha na CD ya ushahidi wote walioutumia kutoa hukumu. Mwandishi wa habari hizi ailizungumza na Shehe Mkuu wa Mkoa ambapo alithitisha shauri hilo kuwepo mezani kwake na kwamba analifanyia kazi.
Mtandao huu pia uilifanikiwa kuzungumza na mdai, Juma ambaye alikiri kumshtaki katibu huyo wa Bakwata mkoa kwa kosa la kuvurunga ndoa yake. Alipotafutwa katibu huyo, hakuweza kupatikana. Jitihada za kumtafuta zinaendelea.