Mashindano ya Kufuzu Afcon kwa Vijana U17 Kuzinduliwa leo

Mashindano ya Kufuzu Afcon kwa Vijana U17 Kanda ya CECAFA Kuzinduliwa leo
Mashindano ya kufuzu Afcon kwa vijana U17 Kanda ya CECAFA (CECAFA U17 Afcon Zonal qualifier ) yanazinduliwa leo Jumamosi,  August 11, 2018 katika uwanja wa Taifa, Dar Es salaam.

Katika uzinduzi, mwenyeji Tanzania atacheza na Burundi katika uwanja wa Taifa, saa 11.00 jioni.

Mashindano hayo yatashirikisha timu za vijana U17 kutoka mataifa tisa katika ukanda wa CECAFA ambayo ni Burundi, Rwanda, Sudani, Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini, Djibouti na mwenyeji Tanzania (Serengeti boys).

Bingwa katika mashindano hayo, ataiwakilisha Kanda ya CECAFA katika fainali za mashindano ya Afcon U17, Africa, mwakani  ambayo mpaka sasa mwandaaji ni Tanzania.

Mashindano hayo Watanzania wenzangu ni muhimu sana, ni muhimu kwa maana ya kupata ushindi (Ubingwa) ili ushiriki mashindano kama hayo Africa.

Iwe, isiwe, tufanye tufanyavyo Tanzania tuwe mabingwa wa mashindano hayo ili tuwe na sifa na uhakika wa kushiriki mashindano ya U17 Africa.

Tusibweteke kusema eti kwakuwa sisi ndio waandaaji wa mashindano ya Africa, tutashiriki kwa mgongo wa uenyeji wetu, tutakuwa tunajidanganya, lolote linaweza likatokea, wakubwa hao wakaamua kutunyang'anya uandaaji, japo hatuombei, tutajuta na kuijutia kuikosa nafasi ya ushiriki kwa kukosa sifa kama hatutakuwa mabingwa wa CECAFA katika mashindano yanayozinduliwa leo katika ardhi ya nchi yetu, Uwanja wa Taifa, Dar Es salaam, AIBU.

Vijana wetu, Serengeti boys, nawaamini sana katika uwezo wa kucheza mpira, naamini hata wewe Mtanzania mwenzangu unaamini hivyo kwani, ni juzi tu wamekuja na kikombe katika mashindano yaliyofanyika nchini Rwanda.

Vijana wetu hawa, wanahitaji hamasa ya ushangiliaji kutoka kwa Watanzania, tuwatie moyo, tujitokeze kwa wingi mno, tushangilie muda wote, wajue tunataka matokeo chanya kwa kila mchezo ili tuwe mabingwa wa mashindano hayo, nina imani umati na ushangiliaji wetu wa nguvu, vijana watafanya kweli, tutakuwa mabingwa, nchi yetu itasifika na kuaminika kwa Soka ulimwenguni, akina SAMATA wataongezeka ULAYA.

TFF kwa kuona umuhimu wa mashindano hayo, wamefanya sehemu yao ili kurahisisha ushindi na upatikanaji wa ubingwa,  mosi, wamepambana na kuwezesha mashindano hayo yafanyike NYUMBANI,  lakini katika kumwezesha kila Mtanzania kuingia uwanjani, wameondoa kiingilio, ni bure kabisa, hata ndururu moja hutoi, ni wewe tu na miguu yako, utaingia uwanjani kupitia geti, mlango utakaoupenda maana, milango yote itakuwa wazi.

Watanzania wenzangu, Mungu atupe nini, ebu tuoneshe kwa vitendo uzalendo wetu, tujitokeze kwa wingi, tuingie uwanjani kwa maelfu,  tuwashangilie vijana, kwa nguvu na umoja wetu, ubingwa utapatikana tu, tutawapapasa kikamilifu, morari ya vijana ikipanda kila dakika kwa makelele ya ushangiliaji kutoka kwa Watanzania wenzao.

Halafu ndugu, Watanzania, Wazalendo wenzangu,  katika ukanda huu wa CECAFA na Africa, Tanzania tunasifika kwa kuwa na mapenzi na mpira wa miguu kwa namna ambavyo tumekuwa tukijitokeza kwa wingi kuzishangilia timu zetu, ebu tusiipoteze sifa hii, mashindano hayo ni makubwa mno, tujitokeze kwa wingi mno, tuwashangilie vijana, watutoe kimasomaso, kikombe kibaki, tuwe na uhakika wa kushiriki Afcon U17 Africa, mwakani.

Kwa Mtanzania, Mzalendo,  mwenye machungu na nchi yake, mwenye kuhitaji mafanikio, hasa katika soka, ni wakati muafaka sana wa kuonesha uzalendo wetu kupitia mashindano hayo, TUJITOKEZE kwa wingi, tuje tuwashangilie vijana wetu kwa nguvu moja ya pamoja, UBINGWA ni WETU.

Adui akikufuata nyumbani si rahisi kukupiga, akikupiga, wewe utakuwa tatizo, maana nyumbani kwako una kila kitu na ziada ya wapiganaji, ukiona Baba umezidiwa , muite mama mmchangie, mtandikeni kwa kila aina ya silaha, mikanda ya suruali ya baba, viatu vya mchongoko vya mama, mwiko wa kusongea ugali, hata wigi la nywele za mama ni silaha imara kabisa kutosha kumuadabisha adui aliyekuvamia nyumbani kwako.

Tayari adui yuko nyumbani kwetu, ebu tumchangie, tumpige kwa kila aina ya silaha tulizonazo ndani mwetu, na katika mashindano hayo, silaha pekee za ushindi ni KUJITOKEZA kwa wingi kwenda uwanjani na KUSHANGILIA, kwisha habari yao.

Shime Watanzania, tuoneshe kwa vitendo kwamba, tunaipenda NCHI yetu, tunaupenda MPIRA, tujitokeze kwa wingi, tuwashangilie SERENGETI BOYS.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad