HITMAKER wa Ngoma ya Nadekezwa ambaye pia ni Memba wa Wasafi Classic Baby (WCB), Mbwana Yussufu ‘Mbosso’, amefunguka kuwa kipindi amepotea kwenye muziki baada ya kuachana na Yamoto Band, licha ya kuendelea kutoa ngoma zake kama msanii wa kujitegemea, kuna baadhi ya media zilikuwa hazichezi na zilitaka kumzika akiwa hai.
Akipiga stori na Star Showbiz, Mbosso alisema kwamba kipindi hicho kilikuwa ni kigumu kwenye maisha yake, kuna muda alikuwa hadi analia, lakini baada ya kuingia WCB, mambo yamebadilika kabisa na kila siku anaona muujiza mpya kwenye kazi yake ya muziki.
“Kiukweli ninamshukuru Mungu anayetoa riziki. Ingekuwa inatolewa na binadamu pengine mimi nisingepata chochote kwa sababu kuna baadhi ya media zilikuwa hazichezi ngoma zangu, zilitaka kunizika nikiwa hai zikiamini kwamba siwezi na sitafika popote pale.
“Lakini Mungu mkubwa, mambo yamebadilika na kwa sasa nipo kazini ninafanya kazi na wanamuziki watano wakubwa Afrika, na kila kitu kikikaa sawa nitaweka wazi,” alisema Mbosso.