Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA Wawekewa Pingamizi

Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA Wawekewa Pingamizi
Jamhuri imepinga maombi ya vigogo tisa wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ya kutaka kesi inayowakabili iahirishwe hadi rufaa isikilizwe na kutolewa uamuzi kwa madai kwamba maombi hayo hayana msingi kisheria.

Hoja hizo za Jamhuri ziliwasilishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi hiyo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, aliomba mahakama hiyo iyatupilie mbali maombi hayo.

Mbowe na wenzake wanaiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo, kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa rufani waliyowasilisha Mahakama ya Rufani Tanzania.

Mbowe na wenzake waliwasilisha maombi hayo kupitia wakili wao Peter Kibatala, wakiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hadi hapo Mahakama ya Rufani itakaposikiliza na kutolea uamuzi rufani watakayowasilisha  kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam wa kutupilia mbali maombi hao ya marejeo.

Pia, vigogo hao wamewasilisha maombi Mahakama ya Rufani wakiomba kusimamishwa kwa mwenendo wa kesi hiyo hadi rufani yao itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Nchimbi alidai wanapinga vikali hoja za waleta maombi (Mbowe na wenzake) kwa kuwa maombi yanakosa baraka za kisheria au yanakosa miguu ya kisheria ya kusimamia mbele ya mahakama.

Alidai maombi hayo hayana kitu kipya kwa kuwa mahakama hiyo ilishatoa uamuzi mdogo kutokana na maombi yaliyokuwa yamewasilishwa na Mbowe na wenzake ya kuomba kusitishwa kwa mwenendo wa shauri hilo.

“Hakuna chochote kipya kilichowasilishwa mahakamani kitakachoifanya mahakama hii itoe uamuzi wa kuahirisha mwenendo wa shauri la jinai,” alidai.

Alisema kifungu kilichotumika kuwasilisha maombi hayo na kesi mbili zilizotumiwa na upande wa waleta maombi huwezi kupata kile alichokiomba.

Kuhusu hoja ya hati ya kiapo kinzani, Nchimbi alidai ipo sahihi na kama ingekuwa na upungufu upande wa wajibu maombi wangewasilisha hoja ya kisheria.

Aliomba mahakama hiyo itupilie mbali maombi haya kwa kukosa misingi ya kisheria.

Wakili Kibatala katika maombi ya wateja wake, aliomba mahakama kuahirisha kesi kwa kuwa kuna rufani Mahakama ya Rufani na wamewasilisha maombi ya kusitisha usikilizwaji wa kesi hiyo.

Kibatala alidai wanaomba kuahirisha kesi hiyo ili kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa rufani iliyoko Mahakama ya Rufani na maombi ya kusimamishwa kwa mwenendo wa shauri hilo kusubiri uamuzi wa rufani.

Alidai kifungu kilichotumika kuwasilisha maombi hayo kinaipa mamlaka mahakama hiyo kuahirisha usikilizwaji wa shauri la jinai kwa kipindi kisichozidi siku 15 kwa mshtakiwa ama washtakiwa walioko mahabusu na kwa kipindi kisichozidi siku 30 iwapo mshtakiwa ama washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Kibatala alidai mamlaka ya mahakama yapo wazi kabisa katika sheria, lakini pia yalisisitizwa na Mahakama ya Rufani katika mashauri mbalimbali.

“Ukichukua hati ya kiapo ambacho ameapa yeye kuunga mkono maombi hayo na hati ya kiapo kinzani, hakuna ubishi kwamba kuna maombi ya kusimamishwa kwa mwenendo wa shauri hilo yaliyoko Mahakama ya Rufani, hakuna ubishi rufani imeshawasilishwa na kusajiliwa.

“Maombi yaliyoko katika Mahakama ya Rufani yanagusa mwenendo wa kesi na kutokana na mchakato wa rufani ulivyokwenda haraka, tunaamini maombi ya kusitishwa kwa mwenendo wa kesi yatakwenda haraka.

“Mheshimiwa hakimu, tuna mashaka na uhalali wa hati ya kiapo kinzani kilichowasilishwa na upande wa wajibu maombi, hati tuliyopatiwa haina saini mwisho wa maelezo wala tarehe,” alidai Kibatala.

Alidai kutokana na hilo, hakuna hati ya kiapo kinzani iliyowasilishwa mahakamani hapo na kuomba maombi yao yakubaliwe.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad