Mbunge Afunguka Jinsi Dereva Wake Alivyokufa Ajalini

Mbunge Afunguka Jinsi Dereva Wake Alivyokufa Ajalini
MBUNGE wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Magereli, amesimulia jinsi dereva wake, Yohana Kagine (42), alivyokufa kwa ajali wakati akimuwahi.

Dereva huyo alikufa kwa ajali wakati akimuwahi mbunge huyo aliyekuwa amekwama alipokuwa njiani kuelekea mkoani Kigoma kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Buyungu.

Akizungumza na Nipashe jana mchana, Magereli alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 9:00 usiku katika Kijiji cha Nkuyi Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati dereva huyo akimfuata ili waendelee na safari ya kuelekea Kigoma.

Alisema gari alilokuwa akitumia dereva wake ni aina ya RAV 4 yenye namba za usajili T 348 CSR ambayo iligongana uso kwa uso nia lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 237 CHE.

Mbunge alisema alitoka jijini Dar es Salaam na kupita Dodoma na wakati akiendelea na safari kuelekea Buyumbu Kigoma kwa ajili ya kampeni za uchaguzi zinazoendelea, alipofika njia panda ya Kahama gari alilokuwa akiitumia ilipata hitilafu.

“Kwa sababu ya majukumu mengi niliyonayo Kigoma, nilimpigia simu dereva Yohana ambaye nilimuacha Dodoma aje Kahama na gari lingine hivyo alikuwa akinifuata anipeleke Kigoma,” alisema.

Aliongeza: “Kwa bahati mbaya akiwa njiani akapata ajali amegongana na Fuso uso kwa uso na kufariki. Magari yote mawili yameharibika na alilokuwa anaendesha Yohana halifai.”

Alisema baada ya kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio na wakati huo alikuwa akielekea hospitali kwa ajili ya kuangalia mwili wa marehemu.

Naye, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Sweetbert Njewike, alisema wakati wa ajali hiyo ikitokea, dereva wa Fuso, Frank Haji (36), mkazi Singida alikuwa akitoka Singida kuelekea Dar es Salaam na Kagine alikuwa akitokea Dodoma kuelekea Singida.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Fuso kuhama eneo lake na kuingia upande wa kulia ndipo alipokutana uso kwa uso na RAV4 na kusababisha dereva Kagine kupoteza maisha hapo hapo.

Alisema dereva wa Fuso aliyesababisha ajali hiyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad