Mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi na viongozi watatu wa mgodi wa Stamigold ulioko Tulawaka wilayani Biharamulo mkoani Kagera, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Biharamulo, Hassan Mosi amesema mbunge huyo na wenzake walikamatwa na kuwekwa rumande katika gereza la wilaya hiyo Jumamosi Agosti 4, 2018.
Amesema leo Jumatatu Agosti 6, 2018 watafikishwa mahakama ya wilaya ya Biharamulo kwa kosa la kufanya miamala ya kupokea rushwa.
Mosi amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha15 cha sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya kupambana na kuzuia rushwa.
"Wakifikishwa mahakamani watasomewa mashtaka yanayowakabili. Wanaweza kukiri au kukanusha na sheria itachukua mkondo wake,” amesema.