Mbwana Samatta Awake Rekodi ya Kipekee KRC Genk, Awazidi Wenzake Waliotimka
0
August 27, 2018
Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amewapoteza mastaa Kevin De Bruyne wa Manchester City na Christian Benteke Crystal Palace kwa kuweka rekodi ya aina yake KRC Genk.
Mabao yake matatu ‘hat-trick’ aliyoyapachika mshambuliaji huyo wa Kitanzania kwenye mchezo uliopita wa kuwania kufuzu Europa Ligi dhidi ya Brøndby yamemfanya kuweka rekodi hiyo tamu KRC Genk.
Achana na ile rekodi ya kuwa hat trick yake ya kwanza, rekodi tamu aliyoweka mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba ni kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Genk katika michezo ya awali ya kuwania nafasi ya kuingia makundi ya Europa Ligi.
Huyo ndiye Samatta aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa ndani kwa wachezaji wa Afrika 2015, mshambuliaji huyo anashikilia rekodi hiyo akiwa na mabao manane.
Wanaomfuatia nyuma ni Jelle Vossen ambaye kwa sasa anaichezea Club Brugge KV, nyota huyo akiwa KRC Genk kwa miaka mitano alitumia mechi tano za mchujo kuingia makundi kwa kufunga mabao matano sawa na winga, Leandro Trossard.
Leon Bailey ambaye alicheza na Samatta na baadaye kujiunga na Bayer 04 Leverkusen ya Ujerumani anayoichezea hadi sasa, yeye anamabao matatu sawa na kiungo Dániel Tőzsér ambaye kwa sasa anaichezea Debreceni VSC ya Uholanzi.
Wengeni wenye mabao mawili, Edon Zhegrova, Ruslan Malinovskyi, Marvin Ogunjimi (Sai Gon FC), Elyaniv Barda ametundika daruga, Thomas Buffel (SV Zulte Waregem) na Sébastien Dewaest.
Wenye bao moja ni Stein Huysegems (FC Berlaar Heikant), Steeven Joseph-Monrose (FK Gabala), Christian Benteke (Crystal Palace), Zinho Gano, Neeskens Kebano (Fulham FC), Kevin De Bruyne (Manchester City), Bryan Heynen na Alejandro Pozuelo.
De Bruyne aliichezea KRC Genk kwa miaka saba kabla ya kutimkia Chelsea, 2012 huku kwa upande wa Benteke aliichezea klabu hiyo kwa miaka mitatu na baadaye kujiunga na Standard Liège.
Samatta anaifukuzia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa KRC Genk, mshambuliaji huyo kabla ya mchezo wa jana wa Ligi Kuu Ubelgiji dhidi ya Waasland-Beveren anajumla ya mabao 41 ambayo ameyafunga katika mashindano yote toka alipojiunga na klabu hiyo, 2016.
Katika orodha ya wafungaji wa muda wote wa KRC Genk, Samatta anashika nafasi ya sita nyuma ya kinara Vossen mwenye mabao 105, mstaafu Wesley Sonck anamabao 80.
Wengine ni Kevin Vandenbergh wa SC Aarschot aliifungia KRC Genk mabao 68, Barda ambaye alishatundika daruga mabao 67 na Buffel anayeichezea SV Zulte Waregem alipachika mabao 59.
Pamoja na Samatta kuifukuzia rekodi hiyo, anasalia kama mfungaji bora wa muda wote wa KRC Genk kwa upande wa wachezaji wanaoendelea kukitumikia kikosi hicho.
Benteke katika orodha ya wafungaji wa muda wote, yupo nafasi ya 17 akiwa na mabao 20 huku kwa upande wa De Bruyne yupo nafasi ya 23 akiwa na mabao 17.
Tags