Mfuko wa Pensheni wa PSSSF Waanza Rasmi Leo

Mfuko wa Pensheni wa PSSSF Waanza Rasmi Leo
Tarehe 31 Januari, 2018 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).



Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inaunganisha Mifuko ya Pensheni minne ambayo ni Mifuko ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF na kuunda Mfuko mmoja kwa ajili ya Watumishi wa Umma unaojulikana kama Mfuko wa Hifadhi kwa Watumishi wa Umma.



Mara baada ya kupitishwa na Bunge tarehe 8 Februari, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alitia saini Sheria hiyo na hivyo kuifanya kuwa sehemu ya Sheria za nchi.



Baada ya kukamilika kwa hatua hizo muhimu, hatua inayokuwa inasubiriwa ni kutangazwa kwa tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF.



Kwa mujibu wa Sheria, Waziri mwenye dhamana ya Hifadhi ya Jamii ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza tarehe baada ya kuridhika kuwa maandalizi yote ya msingi yanayohusu utekelezaji wa Sheria hiyo yamekamilika.



Napenda kuchukua fursa hii kuwajulisha kuwa Serikali imekamikisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji wa Sheria ya PSSSF na imeridhika kwamba Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma( PSSSF) unaweza kuanza kutekeleza majukumu yake.



Napenda kutangaza rasmi kwamba, kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 1(1) cha Sheria ya PSSSF nimeteua tarehe 1 Agosti, 2018 kuwa ndiyo tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF.



Hatua hii inamaana kwamba Mfuko wa PSSSF utaanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 1 Agosti, 2018, hivyo kuanzia tarehe hiyo wafanyakazi wote watakaoajiriwa katika sekta ya umma watasajiliwa katika Mfuko wa PSSSF na wale watakaoajiriwa katika sekta binafsi watasajiliwa katika Mfuko wa NSSF.



Wanachama wote ikiwa ni pamoja na wastaafu na warithi waliopo katika mifuko inayounganishwa watahamishiwa katika mfuko wa PSSSF na haki na stahili zao zitaendelea kutolewa na Mfuko huo bila kuathiriwa kwa namna yeyote ile.



Vivyo hivyo, rasilimali, vitega uchumi, madeni, mifuko ya hiari na mikataba iliyokuwa chini ya mifuko inayounganishwa itahamishiwa katika Mfuko mpya wa PSSSF.



Watumishi wote wa mifuko inayounganishwa watahamishiwa katika mfuko mpya ambako uongozi wa Mfuko huo utawapangia majukumu yao kwa kuzingatia muundo wa Mfuko huu.

Kabla ya kufikia hatua ya kutangaza tarehe ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF, Serikali ilipaswa kuhakikisha kwamba imekamilisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji ili kuhakikisha kwamba huduma kwa wanachama haziathiri kwa namna yeyote ile.



Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Mifuko imeandaa mkakati maalumu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu Sheria na Kanuni za PSSSF ili kuhakikisha kwamba wanachama na wadau wote wa Sekta wanakuwa na uelewa sahihi wa Sheria hizi na mabadiliko yaliyofanyika.

*Imeandaliwa na Idara ya Habari- MAELEZO*
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad