Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mtu mmoja, aliyejulikana kwa jina la Prosper Lema, aliyedai kutekwa na watu wasiojulikana na kuanza kutumia uongo kuomba fedha kwa ndugu zake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, amesema, taarifa hizo za Bw. Lema zilipatikana baada ya ndugu zake mtuhumiwa huyo kwenda katika kituo cha polisi kirumba jijini humo kutoa taarifa ya ndugu yao kutekwa na watu wasiojulikana Julai 18, mwaka huu baada ya kuwatumia ujumbe akiomba fedha.
Kamanda Msangi amesema kwamba mtuhumiwa Lema aliomba fedha zaidi ya shilingi milioni tano kwa familia yake kwa kutuma ujumbe kwenye simu ili aweze kuachiwa huru na watu waliomteka.
Aidha ameongeza kwamba mtuhumiwa Lema atafikishwa Mahakamani pindi uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika.
Mbali na hayo, Kamanda Msangi amewatahadharisha wananchi kuwa makini na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapobaini kuwepo kwa dalili zinazofanana na hizo.