Mshambuliaji wa Liverpool raia wa Misri Mohamed Salah anachunguzwa na polisi baada ya video yake kuibuka akionekana kuendesha gari akiwa bado anatumia simu.
Klabu yake inadaiwa kuwa ndiyo iliyopiga simu kwa polisi.
Polisi wa Merseyside wamethibitisha kupitia ujumbe wa Twitter kwamba video hiyo imekabidhiwa kitengo husika.
Msemaji wa Liverpool amesema waliwafahamisha polisi kuhusu video hiyo baada ya kuzungumza na mchezaji huyo.
Ameongeza kwamba hatua zozote zinazohitajia kuchukuliwa kuhusu tukio hilo zitachukuliwa kwa kufuata mifumo ya ndani.
Video hiyo ambayo imesambazwa sana kwenye Twitter inaonekana kumuonesha mchezaji huyo, akiwa anatumia simu yake akiwa amelisimamisha kwa muda huku akiwa amezingirwa na mashabiki, wakiwemo watoto. Kisha analingurumisha gari na kundoka akiwa bado anaitumia simu yake.
Msemaji wa klabu hiyo amesema: "Klabu, baada ya kushauriana na mchezaji, imewafahamisha Polisi wa Merseyside kuhusu kanda hiyo ya video na matukio yaliyokuwa yanaendelea wakati wa kupigwa kwa video hiyo."