Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema amemtaka waziri wa mambo ndani, Kangi Lugola kuwachukulia hatua wabunge wanaomchafua Rais John Magufuli.
Amesema kuna vikundi vya wabunge ambao wanatengeneza chokochoko dhidi ya Rais na kwamba hatua zichukuliwe kabla hawajatimiza azma yao mbaya dhidi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Agosti 3 katika ofisi za chama hicho zilizopo Magomeni, Dar es Salaam, Mrema amesema wabunge hao ambao baadhi ni wanachama wa CCM wanahatarisha usalama wa Rais kwa kumchonganisha na wananchi.
Mrema ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali ya awamu ya pili amesema anawafahamu wabunge hao licha ya kutowataja majina yao.
Ameahidi kumpa ushirikiano Waziri Lugola endapo atahitaji kwa kuwa anafahamu mambo hayo kiundani.
"Mimi nimewasikiliza wabunge tena wa CCM kwa mfano waliosema Rais amechukua Trilioni 1.5 ni kweli au ni kumchafua? Kwa hiyo kuna hiyo tabia imezuka ya kumzulia Rais maneno ya uongo na ya kumdhoofisha,"alisema.
Alisema vikundi hivyo nimekuwa vikitengeneza "chokochoko" ambazo zinalenga kumchonganisha Rais na wananchi.
"Wabunge hao nawafahamu na niko tayari kuwataja kabla hawajatimiza uovu kama ilivyokuwa kwangu,"amesema.
Alieleza kuwa atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha Rais anaheshimiwa na kuungwa mkono kwa sababu kazi aliyonayo ni kubwa.
Pia amemshauri Rais Magufuli kuwa makini na viongozi wake kwa kuwa wengi wanafanya mambo kwa kutafuta ‘kiki’ na huenda wakawa si rafiki katika kazi zake.