Msanii mkongwe wa filamu bongo, Vincent Kigosi maarufu kama 'Ray' amesema ukimya wake kwenye sanaa ulitokana na yeye kuwa 'busy' na familia yake pamoja na kusoma mapungufu ya wasanii wa sasa huku akidai kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kushinda naye atakaporudi rasmi mwishoni mwa mwaka huu
Ray ametoa kauli hiyo leo Agosti 21, 2018 alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv baada ya ukimya wake kwenye sanaa, takribani miaka miwili jambo ambalo likapelekea mashabiki na wadau wa filamu nchini kudai huenda msanii huyo ameishiwa ubunifu katika kufanya kazi zake.
"Siku zote ukimya una kishindo kikubwa, halafu unapokuwa mtu mzima na makini hupaswi kukurupuka kwa kufanya kazi ili mradi tu uwaridhishe watu, soko limeyumba kidogo kwa hiyo ni lazima ukae chini uangalie ni wapi kuna mistake na marekebisho yake jinsi ya kuyafanya. Kuna vitu vingi vilinifanya niwe kimya lakini mwaka huu hauishi watanzania watapata kile wanachostahili, mimi huwa sibahatishi kwenye kazi zangu. Watu hawataki kujifunza vitu na badala yake wanataka kujifanya wanajua kila kitu, mimi nilikuwa na marehemu Steven Kanumba na tulikuwa washindani katika sanaa", amesema Ray.
Pamoja na hayo, Ray ameendelea kwa kusema "yule mtu mmoja aliyekuwa mshindani wangu amefariki dunia sasa nashindana na nani tena ?, hakuna ushindani tena sasa hivi na ndio maana unakuta soko limeyumba nasio kwamba limeondoka na Kanumba tatizo ni ule ushindani uliokuwa awali sasa hivi haupo".
Aidha, Ray amedai wasanii wa sasa ni wazuri kiasi chake ila kinachokosekana ni ushindani ndani ya tasnia hiyo na kupelekea bongo movie kuyumba kwa namna moja ama nyingine.
Ray Kigosi ni miongoni mwa wasanii wa kongwe nchini Tanzania ambao walianza kujihusisha na sanaa kupitia vipindi vya televisheni, na mwisho wake kuhamia rasmi kwenye ulingo wa filamu.