Mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Itega iliyopo jijini hapa, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu ikiwamo kumkaba na kujaribu kumuibia mama yake mzazi.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kutenda uhalifu huo akiwa na kikundi cha uhalifu cha Kamchape kinachojihusisha na ukabaji na uvunjaji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Gilles Muroto alisema jana kuwa, kijana huyo ni mhalifu sugu na siku za karibuni alimkaba mama yake.
“Lakini mama huyo hakujua kuwa aliyemkaba ni mwanaye, ila huyu kijana alijua kuwa aliyemkaba na kumpora ni mama yake mzazi,” alisema Muroto.
Alisema mwanafunzi huyo alieleza namna alivyomkaba mama yake wakati akihojiwa na polisi.
Muroto alisema katika mahojiano na mwanafunzi huyo, aliwaambia kwamba baada ya kugundua kuwa aliyempora ni mama yake mzazi aliuachia mkoba na kutokomea kusikojulikana.
Alisema kuna wakati alikamatwa kwa uporaji na kuachiwa, lakini amekamatwa tena baada ya kutuhumiwa kuvunja nyumba na kuwafunga kamba wenye nyumba ili awaibie.
Alipoulizwa na Kamanda Muroto mbele ya wanahabari jana kwa nini anajihusisha na makundi ya uhalifu badala ya masomo, kijana huyo alisema anasukumwa na ugumu wa maisha kufanya hivyo.
“Ninaishi na mama peke yake, hivyo sina mtu wa kunihudumia viatu vya shule, madaftari, vitabu, sare za shule na mahitaji mengine. Ndiyo maana nakaba watu ili nipate mahitaji hayo,” alisema Mohamed.
Alisema baba yake amefariki dunia na kwa sasa anaishi na mama.
Polisi wamebaini kuwa vijana wengine wengine wanne wanaounda kundi la Kamchape linalojihusisha na uporaji eneo la Kizota ambapo wote wamekamatwa.
Kamanda Muroto alitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu pamoja na wale wanaonunua vitu kutoka kwa wahalifu kuwa watakamatwa na kufikishwa mahakamani.