Neno la Akili Kwa Mavoko na WCB..."Kuachana Kwa Chuki sio Mpango"


MOSI: WCB wafahamu kuwa Mavoko ana tofauti na wanamuziki wengine ambao inawasimamia. Mavoko ni staa kabla ya WCB. Zipo nyakati CEO wa WCB, Diamond Platnumz, alishindanishwa na Mavoko. Yapo mambo wakifanyiwa akina Lavalava, Harmonize na wengine wanaweza kuvumilia, maana hawajawahi kuuweza muziki nje ya WCB.

Movoko anaujua muziki, faida na hasara zake nje ya WCB. Endapo ataona WCB ni pagumu kuliko kabla hajajiunga na familia hiyo, lazima aamue kuondoka. Ni tofauti na wengine ndani ya WCB, wakisema WCB pagumu, watakuwa wanalinganisha na wapi ambako hawajakuwepo?

Pili: Mavoko na WCB wanategemeana. Awali WCB ilionekana ni lebo ya wasanii wanaoanza fani, lakini kujiunga kwa Mavoko kwenye taasisi hiyo, kulifanya ionekane ni kampuni kubwa yenye kushawishi mpaka wasanii wakubwa. Mavoko akiondoka, itaonekana WCB haiwawezi wakubwa, inamudu vijana ambao hawajajiweza.

Mavoko pia atambue kwamba muziki ni biashara, hivyo matangazo ni muhimu sana. Kabla hajajiunga WCB alikuwa msanii mkubwa lakini hakuwa akiwekwa pazuri kibiashara kutokana na udogo wa promosheni. Baada ya kujiunga WCB biashara yake iliongezeka kwa kiasi kikubwa. Aheshimu kuwa WCB wanazijua njia za kibiashara katika muziki. Kwa maana hiyo akiendelea nao watanufaika.

Tatu; WCB watambue kuwa kwenye muziki hakuna anayeajiriwa. Pande mbili zinaingia mkataba wa kushirikiana kibiashara. Hivyo, WCB na Mavoko ni washirika wa kibiashara (business partners). Mambo eti mtu kakosea unamsimamisha kazi ni utoto. Inapaswa kuangalia mkataba kuangalia mahali palipokiukwa.

Nne; ubinafsi ni sumu. WCB kama wanamhitaji Mavoko ni vizuri wakapitia mkataba wao na kuona jinsi ambavyo kila upande unanufaika. Mpaka Mavoko anaomba mkataba uvunjwe maana yake anaona akiwa nje ya WCB atapata zaidi. Hivyo, wakiketi na kujadili namna ya kuridhiana wanaweza kubaki wamoja.

Tano: mahakamani ni kushinda kila kitu au kupoteza vyote. Wakielewana Basata wataweza kumalizana katika mazingira ya kiungwana. Mahakamani kuna upande utapoteza kila kitu, hivyo kujenga chuki ya kuendelea. Diamond na Mavoko ni wanamuziki na maisha yao ya kimuziki yanaendelea. Hawapaswi kuachana kwa chuki.

By @luqmanmaloto

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad