Mkuu mpya wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo ameapishwa rasmi leo tayari kuanza kuwatumikia wananchi kwa nafasi ya ukuu wa wilaya, ambapo pamoja na mambo mengine amesema ana deni kubwa kwa Rais John Magufuli na wananchi wa Kisarawe.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate amemshukuru Rais Magufuli kwa na nafasi aliyompa ya kuongoza wilaya hiyo na kwamba ana deni
kubwa sana kwa vijana wengi ambao wanamuangalia yeye kama mfano.
Amesema “ sijaja kutengua torati nimekuja kutimilisha, nimekuja kushirikiana na viongozi ambao wamefanya kazi nzuri sana katika wilaya hii ya Kisarawe. Kwa hiyo niseme tu ndugu zangu waandishi wa habari tukutane kazini tuendelee kumsaidia Mh. Rais kuweza kujua maendeleo ambayo tunayafanya kwa ajili ya wananchi tukiongozwa na ilani ya Chama
cha Mapinduzi”
Ni takribani wiki sasa jina la Jokate Mwegelo limejiongezea umaarufu mkubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi baada tu ya jina hilo kutajwa katika orodha ya majina ya wakuu wapya wa Wilaya walioteuliwa na Rais Dkt. John Magufuli.
Ni wazi sasa Jokate Mwigelo ameanza safari yake ya kuwa mtumishi wa umma ambapo baada ya kuapishwa rasmi leo na mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo anakwenda kuwaongoza wakazi 95.614 waliopo katika wilaya ya Kisarawe akiwa kama mkuu wa Wilaya.