Wakati tamasha la Simba Day likifana jana kwa maelfu ya mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi ndani ya dimba la taifa, Dar es Salaam, kuna walakini wa wachezaji wawili kuendelea kuwepo msimu ujao.
Kulia ni kiungo wa Simba Mrwanda Haruna Niyonzima na Mganda Juuko Murshid (kushoto).
Katika tamasha hilo ambalo kufanyika kila mwaka ifikiapo Agosti 8, wachezaji wawili wa timu hiyo, Mrwanda Haruna Niyonzima na Mganda Juuko Murshid hawakutajwa katika orodha ya wachezaji wa msimu ujao.
Wachezaji hao walikosekana katika orodha kutokana na kutokuwepo kwao huku kukizua maswali kama wanaweza wakawepo kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaotaraji kuanza Agosti 22.
Kuchelewa kurejea kwa Niyonzima kumewaacha maswali wanachama na mashabiki mpaka viongozi wa Simba huku kukiwa na hatihati ya uwepo wake ndani ya kikosi cha Simba msimu ujao baada ya kukosekana Simba Day jana.
Ikumbukwe Simba ilitoa likizo kwa wachezaji wake wa kikosi cha kwanza baada ya msimu uliopita kumalizika huku Niyonzima naye alipewa baada ya SportPesa Super Cup kumalizika lakini akashindwa kurejea kwa wakati mwafaka.Hata hivyo Niyonzima bado amesalia na mkataba wa mwaka mmoja ndani ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara ambapo baada ya kujiunga nao alisaini miaka miwili.
Aidha, kuhusiana na Murshid awali uongozi ulieleza kuwa amekwenda Afrika Kusini kukamilisha mipango ya kujiunga na SuperSport United FC lakini baadaye kukaja tena taarifa kuwa ameshindwa kufikia mwafaka na klabu hiyo na ikaripotiwa amesharejea nchini.
Baada ya kuripotiwa kuwa Murushid amesharejea Dar es Salaam, jana katika tamasha la Simba Day naye hakutangazwa na kupelekea kuibua mjadala kama atakuwepo katika kikosi cha msimu ujao.Katika tamasha hilo, Simba ilicheza na Asante Kotoko kutoka Ghana na kwenda sare ya 1-1 huku bao la Simba likiwekwa kimiani na Emmanuel Okwi.